JKCI, UDSM WAZALISHA MASHUJAA WA KUOKOA MAISHA AFRIKA

 

Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akimkabidhi cheti kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge muuguzi ambaye amehitimu mafunzo ya miezi sita ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi kutoka nchini Zambia Angela Mukupa wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha mafunzo hayo leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Jumla ya wauguzi 14 kutoka nchi za Tanzania, Zambia na Rwanda wamehitimu mafunzo hayo.

Mwakilishi wa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Tafiti Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dkt. Leonald Binamungu akimkabidhi zawadi muuguzi ambaye amehitimu mafunzo ya miezi sita ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi kutoka nchini Rwanda Manirakiza Frederick wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha mafunzo hayo leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Jumla ya wauguzi 14 kutoka nchi za Tanzania, Zambia na Rwanda wamehitimu mafunzo hayo.

Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya na Mwakilishi wa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Tafiti Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dkt. Leonald Binamungu wakiwa katika picha ya pamoja na wauguzi waliohitimu mafunzo ya miezi sita ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi kutoka nchi za Zambia, Tanzania na Rwanda leo wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha mafunzo hayo katika Ukumbi wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Jumla ya wauguzi 14 kutoka nchi za Tanzania, Zambia na Rwanda wamehitimu mafunzo hayo. (Picha na: Khamisi Musa)

……………

Na Mwandishi Maalum  – Dar es Salaam

Wahitimu wa mafunzo bobezi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi watu wazima na watoto wametakiwa kutumia maarifa waliyoyapata kama silaha ya kuokoa maisha ya wagonjwa bila kujali hali zao za kiuchumi au kijamii.

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Peter wakati wa mahafali ya sita ya programu hiyo ya miezi sita, yanayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya JKCI na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dkt. Angela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi alisema programu hiyo inayotolewa kwa Wauguzi imekuwa chachu muhimu ya kuimarisha ubora wa huduma za afya hasa katika maeneo ya wagonjwa mahututi na wa dharura, ndani na nje ya Tanzania.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, hususan katika kuendeleza wataalamu na kuimarisha vifaa tiba. Ninyi ni zao la uwekezaji huu. Fanyeni kazi kwa ujasiri, jifunzeni kila siku na muwe tayari kujitolea kuokoa maisha ya wagonjwa,” alisema Dkt. Angela.

Aliongeza kuwa programu hiyo imewajengea uwezo wauguzi kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo Zambia na Rwanda, hali inayoonesha kuimarika kwa ushirikiano wa kikanda katika kuboresha huduma za afya.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Idara ya Utafiti  wa UDSM Dkt. Leonard Binamungu alisema chuo hicho kinajivunia ushirikiano wake na JKCI alisema katika kozi hiyo  UDSM hutoa mafunzo ya nadharia huku JKCI ikitoa mafunzo ya vitendo kwa viwango vya juu vya kitaalamu.

“Ninawapongeza wahitimu 14 mliomaliza mafunzo haya  ambapo wanne wametoka nchini Zambia, Tanzania wanne na Rwanda sita. Nendeni mkawahudumie wananchi kwa weledi, muwe mfano wa kuigwa katika nchi zenu na muendelee kuitangaza Tanzania kama kitovu cha huduma bora za afya,” alisema Dkt. Binamungu.

Naye Mratibu wa Mafunzo hayo Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),  Joshua Ogutu alisema kozi hiyo ni ya miezi sita ambapo wahitimmu hao wamefundishwa jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi kwa watu wazima na watoto.

“Wakufunzi hawa wamejifunza jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi watu wazima na watoto ambao  wamefanyiwa upasuaji wa moyo, mafunzo ya Cathlab  na jinsi  ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaosafishwa damu (Dialysis) ambao figo zao hazifanyi kazi vizuri”, alisema Ogutu.

Nao wahitimu waliomaliza mafunzo hayo walieleza kuridhishwa na ubora wa mafunzo waliyopewa huku wakiahidi kuyatumia kuboresha huduma kwa wananchi.

Afisa Muugunzi kutoka Hospitali ya Moyo Zambia Emanuel Lusale, aliwashukuru wakufunzi  wa kozi hiyo  kutoka JKCI na UDSM na kusema kuwa wamepata maarifa na kujiamini zaidi na wamejipanga kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaowahudumia.

Naye Afisa Muuguzi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Lushoto Magreth Mushi alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa kitaaluma.

“Tunamshukuru Mungu kwa mafanikio haya. Tulianza 14 na tumemaliza wote 14. Mafunzo haya yataboresha kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma kwa wagonjwa wetu,” alisema.

Programu hii inaendelea kuthibitisha mchango mkubwa wa JKCI na UDSM katika kujenga rasilimali watu bora kwa sekta ya afya na kuimarisha ubora wa huduma za tiba ndani na nje ya nchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post