WIZARA YA MALIASILI NA UTALII ILIVYOTAMBA NA HISTORIA YA FARU JOHN NA FARU FAUSTA MBELE YA KAMATI YA BUNGE

Na Mwandishi wetu, Dodoma.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Ashatu Kijaji (Mb) wiki hii ameendelea kuongoza menejimenti ya wizara hiyo mbele ya kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuelezea kazi,majukumu ,muundo na changamoto za wizara hiyo na taasisi zake.

Katika mawasilisho mbalimbali yaliyofanyika mbele ya kamati hiyo kutoka kwa taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikiongozwa na Kamishna wa uhifadhi  Bw. Abdulrazaq Badru iliwasilisha  taarifa yake ikiwa na mafanikio makubwa katika uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.

Katika kikao hicho Ngorongoro iliwakumbusha waheshimiwa wabunge kuhusiana na historia isiyofutika ya faru wakubwa wawili ambao waliishi katika hifadhi hiyo kwa mda mrefu zaidi. Faru hao ni Fausta aliyezaliwa mwaka 1965 na kufa mwaka 2019  na faru John aliyezaliwa mwaka 1978 na kufa mwaka 2016.

Ngorongoro imewaweka kwenye historia  faru hao ili kuwaonesha watanzania umuhimu wa kuhifadhi  faru ambapo idadi yake ndani ya hifadhi hiyo inazidi kuongezeka  na kuvutia  watalii kutoka ndani na nje  ya nchi na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika uingizaji wa fedha za kigeni.

Faru John  ndani ya hifadhi ya Ngorongoro  alijulikana pia  kama Bingwa wa mapenzi ama dume la mbegu kutokana na kuweza kuizunguka hifadhi yote akitafuta faru  majike  ili aweze kushiriki nao tendo la ndoa huku upendo wake ukitawaliwa na wivu wa kupindukia.

Tabia nyingine ya faru  huyo   ilikuwa ni  utawala wa muda mrefu ndani ya hifadhi  hivyo alikuwa  chanzo kikubwa cha migogoro na kutaka kila faru jike awe naye peke yake hali ambayo mwaka 2011 alimuua faru  CHAUSI  kwa kugombea jike hii inadhihirisha ni jinsi gani mapenzi yanaua.

Tofauti na faru John, Faru Fausta, ndiye  faru pekee aliyeweza kuishi ndani ya hifadhi  ya Ngorongoro kwa muda mrefu wa miaka 54 na inasemekana pia amevunja rekodi  ya kidunia kuwa miongoni mwa faru wachache weusi walioweza   kuishi miaka mingi.

Faru  Fausta licha ya kupandwa na madume mbalimbali ikiwenmo faru John, hakubahatika kupata mtoto na kwa  mujibu wa wataalam wa wanyama  haikubainika ni kwanini faru Fausta katika umri wake wote wa miaka 54 hakujaaliwa  uzazi.

 Kisayansi faru anaweza asipate mtoto kutokana na kuwa na matatizo katika mfumo wa uzazi  ikiwa ni pamoja na kuchelewa kupata mimba ambapo faru akiwa na hali hiyo katika  umri unaotakiwa  anakuwa na homoni kiasi kidogo za jike na hivyo kushindwa kupata mimba.

Wataalam wanasema kuwa Faru Fausta inawezekana aliishi muda mrefu kwa sababu hakuwa na msongo wa mawazo wa  kushika mimba,kulea watoto wala kunyonyesha zaidi ya kula bata na kushiriki mapenzi na faru wenzake.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post