📌 Mradi umefadhiriwa na REA na kutekelezwa na TPDC
📌 Mradi umekamilika asilimia 100 na kaya 470 zimeunganishwa na mabomba ya gesi asilia mkoani Lindi
📌 Wananchi wahamasishwa kujiunga katika mradi huo
Mwandishi Wetu Lindi,
Wataalamu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), tarehe 21 Januari, 2026, wametembelea wananchi wanufaika wa Mradi wa Kusambaza Gesi Asilia katika kata za Mingoyo na Mnazi Mmoja mkoani Lindi kwa lengo la kuhamasisha wananchi zaidi kujiunga katika mradi huo ambao umekamilika.
Wananchi wanaonufaika na mradi huo wameeleza kufurahishwa na faida wanazopata baada ya kufikishiwa miundombinu ya gesi asilia hadi majumbani mwao. Bi, Mebo Mkomola, mmoja wa wanufaika, amesema matumizi ya gesi asilia yamerahisisha maisha yake na kuboresha uchumi wa familia yake, ikilinganishwa na changamoto walizokuwa wakikumbana nazo walipokuwa wakitumia kuni na mkaa.
Kwa upande wake, Bi. Zuhura Mbulika (Mama wa familia) amesema gesi imesaidia kupika kwa haraka zaidi ikilinganishwa na matumizi ya mkaa na kuni. Amesema ameshangazwa na baadhi ya watu wanaoamini kuwa chakula kilichopikwa kwa kutumia jiko la gesi asilia si kizuri ukilinganisha na chakula kilichopikwa kwa jiko la kuni au mkaa.
“Chakula kinachopikwa kwa jiko la kuni mara nyingi hunuka moshi au kuungua, huku jiko la gesi asilia hunipa uhuru wa kudhibiti moto kulingana na aina ya chakula,” amekaririwa Bi. Zuhura Mbulika.
Mradi huo umegharamiwa na Serikali kupitia REA kwa shilingi bilioni 6.8 ambapo TPDC imetekeleza kwa kujenga miundombinu (Bomba kubwa la gesi asilia) kutoka chanzo cha gesi eneo la Msimbati hadi kituo cha kwanza cha kupoza na kusambaza gesi kwa mgandamizo mdogo eneo la Mahumbika mkoani Lindi.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kutembelea eneo la Mradi kata ya Mnazi Mmoja, Mhandisi Emmanuel Yesaya, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka REA, amesema jumla ya kaya 470 tayari zimenufaika na mradi huo, akiongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Amesema REA na TPDC wametembelea na kukagua Mradi wa Kusambaza Gesi Asilia ya Kupikia Majumbani kuanzia eneo la Mahimbila mkoani Lindi, ambako kuna mitambo ya mgandamizo wa gesi. Amesema mradi huo unalenga kuwafikia wananchi wanaoishi pembezoni mwa njia ya gesi ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo kwa matumizi ya kupikia, huku ukisaidia kupunguza matumizi ya nishati zisizo safi na salama kama kuni na mkaa.
Mhandisi Yesaya ameongeza kuwa REA imetoa shilingi bilioni 6.8 ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo katika mikoa ya Pwani na Lindi, akisisitiza kuwa matumizi ya gesi asilia yamepunguza gharama za nishati kwa zaidi ya asilimia 60 kwa wananchi waliokuwa wakitegemea nishati zisizo safi kama kuni na mkaa.
Amesema kwa sasa gharama za matumizi ya gesi ni nafuu, ambapo shilingi 1,000 huwezesha matumizi ya mita moja ya ujazo wa gesi asilia (cubic meter 1), hali inayopunguza mzigo wa maisha kwa wananchi.
Ametoa wito kwa Wananchi kubadilika na kuachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama, akisisitiza kuwa matumizi ya gesi asilia huongeza ubora wa chakula, hupunguza gharama za matumizi, na kulinda afya pamoja na mazingira.
Kwa upande wake, Mhandisi Anord Katani, Msimamizi wa Miundombinu ya Gesi Asilia katika Kituo cha Mahumbika, Mnazi Mmoja mkoani Lindi, amesema mitambo iliyofungwa ni ya kisasa na salama kwa matumizi ya nyumbani. Amesema gesi asilia ni nyepesi kuliko hewa, hivyo huongeza usalama endapo kutatokea changamoto wakati wa matumizi.
Naye Kaimu Meneja wa Biashara wa Gesi Asilia kutoka TPDC, Mhandisi Denice Byarushengo, amesema mitambo ya kupunguza mgandamizo wa gesi iliyowekwa imesaidia kufikisha kiwango sahihi cha gesi kinachohitajika kwa matumizi ya nyumbani.
Katika utekelezaji wa mradi huo, Shule ya Msingi na Awali ya Great Minds mkoani Lindi pia imenufaika kwa kufikishiwa gesi asilia.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Magret Nko, amesema mradi huo umesaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa shule, huku wanafunzi wakipata chakula kwa wakati na katika mazingira safi na salama, tofauti na awali walipotumia nishati nyingine.






