Mwandishi Wetu,
Kutokana na uwepo wa changamoto ya uelewa mdogo miongoni mwa wazalishaji wa malisho ya mifugo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, kumekuwepo na upatikanaji mdogo wa malisho ya kutosha na yenye ubora kwa wafugaji, hali inayochangia kushuka kwa tija ya uzalishaji wa mifugo na kuathiri maendeleo ya sekta ya mifugo kwa ujumla.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imeandaa mpango maalum wa utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea katika uzalishaji wa malisho ya mifugo, wenye lengo la kuwawezesha wafugaji na wazalishaji wa malisho kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa malisho na hatimaye kuongeza tija na faida katika ufugaji.
Hayo yamebainishwa jana tarehe 19 Januari, 2026 wakati wa kikao kilichofanyika katika Ofisi ya TALIRI mkoani Dodoma, ili kujadili namna bora ya kutekeleza mpango huo kwa ufanisi kwa kuwafikia wafugaji na wazalishaji wa malisho nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Komba, amesema, moja ya majukumu ya Taasisi hiyo ni kuhakikisha upatikanaji wa malisho na mbegu bora za malisho kwa ajili ya ufugaji wenye tija, hivyo utekelezaji wa mpango huo ni hatua muhimu kwa taifa.
Prof. Komba ameongeza kuwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima na wafugaji ina mchango mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa malisho bora na kuongeza uzalishaji wa mifugo nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa TFRA, Bi. Happiness Mbele, amesema, utekelezaji wa mpango huo utahusisha uainishaji wa mbolea zinazofaa kwa uzalishaji wa malisho pamoja na kubaini mahitaji halisi ya wafugaji na wazalishaji wa malisho.
Ameongeza kuwa, mpango huo pia utajumuisha uanzishaji wa mashamba darasa ya malisho na utoaji wa mafunzo kwa wafugaji na wazalishaji wa malisho ili kuongeza tija na ubora wa uzalishaji.
Bi. Happiness amesema, utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa malisho, kuboresha ubora wa lishe ya mifugo, kupunguza migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, pamoja na kuimarisha utunzaji wa mazingira nchini.



