Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii na Mwenyekiti wa Kamati ya Kuitaingaza Tanzania ya Royal Tour, Dkt. Hassan Abbasi amesema wakati Tanzania imetimiza mwaka mmoja toka Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan atoke ofisini na kucheza filamu ya Royal Tour, kumezaliwa mazao mbalimbali ya utalii hapa nchini.
Dkt. Abbasi ametoa kauli hiyo leo Mei 1, 2023 wakati akihitimisha mjadala wa kitaifa kwenye mtandao (Zoom Meeting) uliojumuisha wadau mbalimbali wa utalii duniani na kurushwa mubashara ya mitandao na vyombo mbalimbali vya habari ulioangazia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa Royal Tour.
Amesema kutokana shuhuda nyingi zilizotolewa na wadau kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi kifupi tangu Roal Tour ilipozinduliwa inapaswa kila mtanzania kuwa balozi wa kuitangaza Tanzania ikiwa ni mkakati wa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita ya kutangaza vivutio vya utalii kwa maslahi ya watanzania na Taifa kwa ujumla.
Pia amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa maono yake ya kuifungua Tanzania duniani kupitia Filamu hiyo na kupongeza balozi za Tanzania katika mataifa mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kuitangaza vivutio vya utalii.
Amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Waziri Mohamed Mchengerwa itaendelea kushirikiana na wadau wote wa utali katika kutangaza mazao yote ya utalii badala ya kutegemea mazao ya awali pekee ya utalii wa Wanyama.
“Nilipata bahati ya kushiriki kwenye mkutano wa dunia ambapo mkutano ule ulihitimisha kuwa kwa sasa uzoefu ndiyo msingi wa utalii, hivyo basi tutaendelea kutoka katika dhana ya kutegemea utalii wa aina moja na badala yake kutakwenda mbali zaidi hadi kwenye utalii wa utamaduni kwa kuwa nchi yetu ina hazina kubwa wa utamaduni”. Amefafanua
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imeandaa mkakati wa kutengeneza mabalozi wa kutangaza utalii wa Tanzania kwenye makundi mbalimbali duniani.
Kamishna wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Wiliam Mwakilema ametoa ushuhuda kuwa filamu ya Royal Tour imeleta matokeo chanya katika eneo la kuongezeka mapato na wageni katika hifadhi zile mbili za Kilimanjaro na Serengeti ambazo Mhe. Rais alipita kucheza filamu hiyo.
Kwa upande wake Fatuma Hamis ambaye ni Katibu Mkuu anayeshughulikia sekta ya Utalii Zanzibar amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano zitaendelea kushirikiana na wadau wa utalii ili kuutangaza utalii wa Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha kuhudumia watalii (TATO) Sirili Akko amefafanua kuwa kutokana na Royal Tour watalii wameanza kurudia safari za kuja nchini huku wakiongeza siku za kukaa ambapo pia amesema filamu imeleta hamasa kubwa na kufanya Taasisi za Serikali kuwa karibu na vyama mbnalimbali vya utalii.
Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri amesema ujio wa Royal Tour umefanya usajili wa uwekezaji kuwa mara dufu katika kipindi hiki huku kukiwa na ongezeko la mtawanyiko wa uwekezaji katika mikoa zaidi ya Dar es Salaam na Arusha iliyokuwepo hapo awali.