WAZAZI WAHIMIZWA KUWAUNGA MKONO WATOTO KATIKA MICHEZO

 Na Shamimu Nyaki


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, ametoa wito kwa wazazi kuunga mkono watoto wanaojishughulisha na Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwa ni miongoni mwa shughuli zenye fursa na ajira kwa waoto hao.

Mhe. Chana ametoa wito huo Aprili 29, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Michezo ya Shule ya Msingi na Sekondari Tusiime ambapo amewahimiza walimu  kufuata ratiba ya Michezo na Sanaa shuleni ili wanafunzi wapate nafasi ya kuendeleza vipaji vyao.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika kuibua vipaji mbalimbali vya Michezo na Sanaa kwa watoto na vijana wetu, na hii ni kutokana na ukweli kwamba kwa sasa duniani kote michezo ni ajira na inaleta faida kubwa kwa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla", alisema Mhe. Chana

Ametumia nafasi hiyo kuikumbusha jamii kuzingatia malezi mema ya watoto, kupambana na mmomonyoko wa maadili, kuzungumza nao kuhusu aina ya marafiki na watu wengine wanaokutana nao katika mazingira yanayowazunguka ili kuwalinda.

Awali Mkugenzi wa Shule za Tusiime, Dkt. Albert Katagira amesema kuwa, lengo la kuwa na siku ya michezo shuleni hapo ni kutoa nafasi kwa wanafunzi kuonesha vipaji vyao ili kuviendeleza viweze kusaidia Taifa kwa ujumla, ambapo amesema shule hiyo ina timu zinazoshiriki ligi mbalimbali za mpira wa kikapu pamoja na vijana wawili ambao wanashiriki michezo nchini Afrika Kusini.

Siku hiyo ya michezo shuleni hapo imejumuisha michezo mbalimbali ya mpira wa pete, mpira wa kikapu na wa miguu ambapo washindi wameibuka na zawadi.

Post a Comment

Previous Post Next Post