DKT, ABBASI - TOUR GUIDE MNA DHAMANA KUBWA KWENYE UTALII

 

Na John Mapepele

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amefunga mafunzo maalum ya siku nne ya uongozaji wa utalii kwa zaidi ya Waongoza Utalii 1300 kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa yaliyoratibiwa na Hifadhi za Taifa (TANAPA)  huku akiwataka kuzingatia utaalam wa fani ya uongozaji wa utalii ili kuboresha  huduma kwa watalii na kuwavutia kuja  kutembelea   vivutio  mbalimbali vya utalii  hapa nchini.


Dkt. Abbasi amefunga mafunzo hayo jijini Arusha leo Aprili 30, 2023 huku akisisitiza kuwa  waongoza utalii ni nguzo muhimu  katika  mnyororo wa thamani  wa Sekta ya Utalii ambapo amesisitiza kuwa  wanadhamana  kubwa ya kuhakisha   huduma inatolewa  kwa kiwango cha kimataifa ili kuwafanya watalii kutoka  maeneo mbalimbali kurejea mara kwa mara nchini hatimaye  kukuza vipato vyao na uchumi wa Taifa kwa ujumla.


“Ndugu zangu hapa naomba niseme tu kuwa sisi waongoza utalii  ndiyo watu ambao tunaweza tukawafanya wageni waendelee kuja  kutuletea fedha ama la  hivyo nitoe wito  kwenu  kuona kwamba kazi yenu ni ya thamani kubwa  katika taifa letu ndiyo maana  hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano alitoka  ofisini akacheza  filamu ya Royal tour kwa  kutambua  thamani ya uongozaji utalii, acheni kulia lia”. Amefafanua Dkt. Abbasi


Aidha, amesema  waongoza utalii wanatakiwa  kuondokana na dhana  ya kuwa  wao  ni watu wa  kawaida  na  badala  yake  kuunga mkono juhudi za Serikali za  kuhifadhi raslimali zilizopo  kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye  pia kuutangaza utalii.


“Katika kipindi cha sasa dhamira ya serikali inakwenda kujikita katika nguzo  mbili kubwa  kuhifadhi na  kutangaza  kwa nguvu zote  vivutio  mbalimbali  vya utalii ambayo nchi yetu  imebarikiwa kuwa navyo  kila kona”. Amesisitiza Dkt. Abbasi

Akimkaribisha Dkt. Abbasi kufunga mafunzo hayo Mtendaji Mkuu wa TANAPA, William Mwakilema amesema  semina  hiyo  imeratibiwa ili  kuwajengea uwezo waongoza utalii wakati huu msimu wa utalii unavyoanza  kufunguka ili wageni  wanapofika waweze  kupatiwa  huduma bora.

Aidha amesema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa kwenye mafunzo hayo ni pamoja na  wajibu wa waongoza utalii, changamoto  za utalii katika  vivuko  vya Nyumbu Mto Mara Kaskazini mwa Hifadhi  ya Taifa  ya Serengeti, Ifahamu Mkomazi na uewekezaji kupitia mfuko wa Umoja Trust Fund kwa waongoza utalii.



 Amesema  kwa sasa  mpango wa TANAPA ni kufungua mbuga  na hifadhi tano zaidi ili nazo zijulikane kama zile kongwe, ambapo amezitaja  hifadhi hizo kuwa ni Mkomazi ambayo itatangazwa  kwa  kauli mbiu  ijulikanayo kama Discover Mkomazi, Sadani, Mikumi,Ruaha  na Nyerere.
 

Akisoma risala kwa niaba ya waongoza utalii wote  Ridas Michael Laizer ameiomba Serikali pamoja na mambo mengine  kuwasaidia waongoza utalii kupatiwa  bima ya afya ambapo Katibu Mkuu amemwelekeza Mkurugenzi wa Idara ya Utalii kukaa chini  na viongozi wa waongoza utalii kujadili kwa kina  changamoto zote na kuzipatia ufumbuzi katika kiopindi kifupi ambapo  pia amesisitiza kuwa viongozi wakuu wa Wizara wanazungumza  na kujadiliana kwa kina na kila kundi kwenye mnyororo wa thamani wa  Sekta ya Utalii ili kuendeleza sekta.

Post a Comment

Previous Post Next Post