Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) jijini Dodoma.
Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya TFRA wakimsikiliza waziri wa Kilimo (hayupo pichani) wakati wa uzinfuzi wa bodi hiyo Machi 31 Mwaka huu jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA Dkt Anthony Diallo nyaraka muhimu za taasisi hiyo ikiwa ishara ya uzinduzi wa bodi hiyo tarehe 31 Machi Mwaka huu.
Waziri wa kilimo (mwenye kanzu nyeusi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo tarehe 31 Machi Mwaka huu jijini Dodoma.
………………,…..
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuwafutia leseni wazalishaji wote nchini watakao bainika kuzalisha mbolea zilizo chini ya kiwango.
Pia Waziri Bashe alisema kuwepo kwa mbolea zilizo chini ya viwango kunapunguza tija kwenye shughuli za kilimo.
Waziri Bashe aliyasema hayo tarehe 31 Machi, Mwaka huu wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA ikiwa ni bodi ya nne tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo mwaka 2012.
“Hatuwezi kuruhusu kuwepo kwa mbolea zilizo chini ya viwango ambazo zitaathiri uzalishaji kwa mkulima hivyo TFRA munapobaini hilo musisite kumfutia leseni mzalishaji
huyo”alisema Bashe
Alisema muuzaji au mzalishaji anapokutwa na mbolea iliyo chini ya viwango kumtoza faini tu haitoshi na wala sio suluhisho, bali TFRA munapaswa kuwa wakali kwani ni bora kumfungia biashara kama hawezi kufuata taratibu” Aliendelea kusisitiza Waziri Bashe
Waziri Bashe aliitaka Bodi hiyo iliyoteuliwa kuhakikisha kuwa matumizi ya mbolea yanaongezeka kutoka Kilo 19 kwa hekta mpaka kufikia kilo 50 na kueleza ongezeko hilo litaleta matokeo chanya kwenye uzalishaji.
Aidha, aliitaka bodi hiyo kuhakikisha inasimamia suala la usajili wa wakulima na hivyo kuwezesha uwepo wa kanzi data inayowatambua wakulima wote nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt. Anthony Diallo alitoa shukrani zake kwa niaba yake na wajumbe wote wa bodi kwa kuaminiwa na kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya kuisimamia na kuishauri Mamlaka yenye dhamana nchini.
Aidha, Dkt. Diallo aliahidi kuwa, bodi yake itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa tasnia ya mbolea inatatua changamoto za wakulima na hivyo kuleta manufaa kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Alisema, yeye na bodi yake wataisoma sheria ya mbolea pamoja na Mpango Mkakati wa Taasisi ili waweze kuyaelewa na kuyasimamia vyema majukumu waliyopewa.
Kufuatia wito wa Waziri Bashe wa kuondoa bidhaa feki kwenye sekta ya kilimo, Dkt. Diallo alisema bodi yake kwa kushirikiana na Menejimenti ya TFRA watakuwa macho kuhakikisha kuwa malalamiko ya wananchi yatokanayo na mbolea iliyo chini ya viwango yanapungua.