Na Jane Edward, Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt Pindi Chana amepiga marufuku matumizi ya moto katika maeneo ya Hifadhi nchini ambayo inatumika kusafisha mashamba na badala yake zitumike mbinu mbadala ili kuzuia mioto inayotokea katika Hifadhi na kusababisha hasara kwa serikali.
Balozi Dkt Pindi akizungumza jijini Arusha wakati akizindua Bodi ya nne ya Wakala wa Huduma za Misitu nchini TFS,amesema kwa sasa satelite inaonyesha kuwa kipindi hiki si rafiki cha kuchoma mioto kutokana na kuwepo kwa upepo mwingi.
Amesema wapo baadhi ya wananchi wanavamia maeneo ya hifadhi na kufanya shughuli ambazo haziruhusiwi hali inayopelekea kuharibika kwa misitu ambayo ndiyo rasilimali muhimu hapa nchini.
"hivi karibuni baadhi ya wafugaji na wakulima wamekuwa wakiingia katika maeneo ya misitu yaliyohifadhiwa kinyume cha taratibu na kulisha mifugo pamoja na kufanya shughuli za kilimo na kuchoma mkaa katika maeneo hayo jambo hili tulikatae kwa dhati kabisa "Alisema Dkt Chana
Amesema endapo misitu ikaachwa kuendelea kulindwa Hali itakuwa si nzuri kwasababu nchi itakosa mvua,majangwa yatatokea na hivyo ni wajibu wa TFS pamoja na bodi yake kuhakikisha hali hiyo inaisha kabisa.
Awali akizindua bodi ya wakala wa misitu Tanzania TFS Waziri Dkt Pindi Chana anasema kwa sasa wajikite katika kusimamia misitu kwa kuwa kwa sasa watanzania wapo zaidi ya Milioni 55 na hatua madhubuti zisipo chukuliwa hali haitakuwa nzuri.
Amesema anaielekeza bodi ya TFS kuhakikisha utalii wa mali kale na ikolojia unaboreshwa ikiwa ni katika kuboresha utalii hapa nchini na pato la Taifa kutopungua Bilioni 6.
Dkt Chana anasema bodi hiyo inatakiwa kutambua mfumo wa kijeshi katika wizara ya Maliasili na utalii ambapo TFS imeanza kutekeleza jambo hilo.
Bregedia Jenerali Mbaraka Mkelemi Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri TFS anatumia nafasi hii kumuhakikishia Waziri kuwa wako tayari kukuza TFS katika masuala mbalimbali .
"katika maelekezo uliyotoa Mheshimiwa Waziri tunakuahidi kuyafanyia kazi na hatutakuangusha kwa wakati mwingine ukija hatutakuwa moja kati ya wanaokwamisha bali yatakuwa ni mafanikio tu"Alisema Bregedia Jenerali Mbaraka
Mwenyekiti anasema bodi hiyo iliyozinduliwa leo itaendelea kutafuta vyanzo vya mapato ili kuendelea kuingizia TFS mapato mengi kuliko kutegemea chanzo kimoja.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa idara ya misitu na nyuki ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambapo ameitaja bodi hiyo kuwa ni imara na italeta tija kubwa kwa Wizara na nchi kwa ujumla.
Amesema bodi hiyo ina watu wenye taaluma mbalimbali kwahiyo mategemeo makubwa ni kuhakikisha TFS inaenda Kimataifa.
Waziri wa maliasili na utalii Balozi Dr Pindi Chana akizungumza jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa bodi ya TFS.
Bregedia Jenerali Mbaraka Mkelemi Mwenyekiti wa Bodi ya nne ya TFS akipokea vitendea kazi kutoka kwa waziri wa maliasili na utalii.