Hali ya upatikanaji mbolea mkoani Mara inaridhisha






 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo ameridhishwa na hali ya upatikanaji wa mbolea katika Mkoa wa Mara.

Dkt. Ngailo ameonesha kuridhishwa huko baada ya kutembelea vituo vitatu vya uuzaji wa mbolea chini ya  Wakala wa Mazao Mchanganyiko (CPB) vilivyopo  wilaya za  Rorya  na Tarime na kubaini uwepo wa shehena za kutosha za mbolea za kampuni za Yara, ETG na OCP.

Pamoja na kujiridhisha na upatikanaji wa mbolea, Dkt. Ngilo amekagua maghala yaliyoainishwa na maafisa kilimo wa Mkoa wa Mara  na wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya katika kijiji cha Kogaya Kata ya Ikoma yenye lengo la kuziwezesha kampuni za mbolea kutunza mbolea hizo kwa msimu wa kilimo 2022/2023 na hivyo kupanua wigo wa kufikisha mbolea kwa mkulima, kupunguza gharama za uendeshaji kwa kampuni la mbolea na hivyo kuipunguzia mzigo serikali.

Akizungumzia kuhusu ukomo wa ekari anazotakiwa kusajiliwa mkulima, Dkt. Ngailo amesema mkulima yeyote anaruhusiwa kusajiliwa kwa heka zozote anazolima ili mradi shamba lisiwe pori aidha wakulima waliopo kwenye vyama vya ushirika (Amcos) au vilivyosajiliwa kwa umoja vinasajiliwa kwa kuweka taarifa za usajili wa vyama hivyo na ekari zinazolimwa. 

Kuhusu uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima, Dkt. Ngailo amesema jitihada za wadau wote wa kilimo zinahitajika na kueleza nia ya kuyaomba makampuni ya mbolea kuwa na mashamba darasa katika maeneo mbalimbali mkoani humo ili kutoa hamasa kwa wakulima kutumia mbolea.

Akizungumza katika kikao baina ya Mkurugenzi Dkt. Ngailo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi  Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mara Levin Magera ameiomba TFRA kufanya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea katika mkoa huo kufuatia wananchi wake kuamini mbolea za viwandani zina madhara kwa udongo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma I. Chikoka amesema awali wakulima hawakuwa na imani yakupata mbolea na hivyo kuwa na mwitikio mdogo wakati wa kujisajili lakini baada ya mbolea kufika wengi wamejitokeza kujisajili na wamenufaika na mbolea za ruzuku.

Chikoka amesema, kwa upande wake anaamini wakulima wa Rorya wakitumia mbolea matokeo ya mavuno yatakuwa makubwa  na kusema mafanikio hayo yanatokana na  juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinua Sekta ya Kilimo nchini.  

Chikoka ameshauri kuendelea kuboresha miundombinu ya usambazaji na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha jambo hili. “Mbolea ipatikane na usambazaji uwe rafiki nasi tunaahidi tutashirikiana kuhakikisha wakulima wapo salama” Mkuu wa Wilaya Chikoka alikazia.

Mkurugenzi Dkt. Ngailo akiambatana Kaimu Meneja wa TFRA Kanda ya Ziwa Khanafi Mohamed amekuwa kwenye ziara ya kikazi kufuatilia upatikanaji na mwenendo wa upatikanaji wa mbolea kwa wakulima pamoja na kubaini maghala yanayoweza kutumiwa na kampuni za mbolea za Yara na Wakala wa Mazao Mchanganyiko (CPB) kusogeza mbolea karibu na wakulima  katika mikoa ya Kagera, Geita na Mara.

Post a Comment

Previous Post Next Post