TEMESA WAKUTANA NA WADAU KUJADILI UBORESHAJI UTENDAJI KAZI

 Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) umekutana na wadau kujadili namna bora ya utoaji wa huduma ili kuleta tija, kupunguza malalamiko ya wateja na kuleta mabadiliko na matokeo chanya kuanzia kwenye menejimenti hadi watumishi.


Kikao hicho kilifanyika Mkoani Morogoro, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Bwana Ludovick Nduhiye, alisema lengo la kikao hicho ni kupitia na kukusanya maoni kuhusu andiko la mkakati wa maboresho ya wakala huo.

Alisema karakana zisizo na ufanisi zinaleta gharama kubwa kwa Serikali katika uendeshaji wake, hivyo wanapitia upya utendeji wa TEMESA ambao utashirikisha pia sekta binafsi ambao ni wadau muhimu.

“Nimefurahishwa sana kuona Mkurugenzi Mkuu wa Toyota kuwa hapa kwani kampuni hiyo ni mdau mkubwa wa Serikali kwenye aina ya magari yanayotumika serikalini pamoja na matengenezo ya magari,” alisema Bwana Nduhiye.

Aliongeza kuwa Serikali imekutana na wadau wake muhimu ili waweze kutoa mtazamo wao kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi hiyo, pamoja na kupokea maoni ambayo yanaweza kutoa majawabu sahihi.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala, alisema ana imani kuwa baada ya kuchambua na kuangalia maeneo mbalimbali ya kufanyia maboresho wakala huo utakuja kivingine na kuendana na kasi ya Serikali katika ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Toyota Tanzania, Bwana Kadiva William, alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa wako tayari kama wadau ambao ni waagizaji wakubwa wa magari yanayotumika serikalini kuisaidia Serikali katika namna bora ya kuvilinda vyombo hivyo ili viendelee kuwa katika hali nzuri na kuiwezesha serikali kupunguza matumizi katika eneo hilo.

Pia aliahidi kuendelea kutoa matengenezo kwa magari mapya hadi yatakapofikia kilometa 76,000 bila gharama yoyote.


Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi Bw.Ludovick Nduhiye akiteta jambo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Bw. Lazaro Kilahara (wa katikati) wakati wa kikao cha wadau cha kupitia na kukusanya maoni kuhusu andiko la mkakati wa maboresho ya wakala huo, Mkoani Morogoro.



Baadhi ya wadau wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi) wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi, Bw. Ludovick Nduhiye (Hayupo Pichani) wakati wa kikao cha wadau cha kupitia na kukusanya maoni kuhusu andiko la mkakati wa maboresho ya wakala huo, Mkoani Morogoro.

PICHA NA WUU

Post a Comment

Previous Post Next Post