Mhe. Mchengerwa amwaga vifaa vya michezo shule zote wilaya ya Rufiji, aanzisha ligi ya Sensa


Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Rufiji.  Mhe, Mohamed Omary Mchengerwa ametoa vifaa vya michezo kwa shule zote za msingi na Sekondari na wanafunzi wanamichezo wote  wanaoshiriki kwenye mashindano ya michezo kwa shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Mashindano  ya Shule za Sekondari (UMISSETA) kwa mwaka 2022 Wilaya ya Rufiji.

Mhe. Mchengerwa amekabidhi  vifaa hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Julai 17, 2022 kwenye  shule ya Sekondari ya Ikwiriri   Wilaya ya Rufiji ambapo amesema ameamua  kufadhili vifaa hivyo katika Wilaya ya Rufiji ili kuiendeleza michezo kwa kuwa michezo ni biashara  na ajira kubwa  kwa vijana.

“Nimeamua kusaidia vifaa hivi kwakuwa natambua  kwa sasa michezo ni miongoni mwa chanzo cha ajira na biashara kubwa duniani hivyo ni vema kufanya michezo kwa umakini mkubwa ili kujipatia ajira” amefafanua

Amewataka wachezaji hao kuwa na nidhamu na kujituma kwa kufanya mazoezi ili waweze kushinda kwenye  mashindano mbalimbali.

“Nendeni mkajitume, michezo ni ajira na  furaha wasikilizeni walimu wenu,  hata shuleni  mtafanya  vizuri”amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Aidha amesema dhamila ya Serikali kwa sasa  ni kuendeleza michezo ambapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazofanya kwenye michezo  katika kipindi kifupi cha utawala wake ambazo zimeleta  mapinduzi makubwa kwenye sekta  hiyo.

Vifaa hivyo vimegharimu zaidi ya milioni 23 ambazo zimenunua zaidi ya jezi seti 200, trakisuti pea 100, kofia 200 na mipira 100.

Pia amefadhili Ligi ya mpira wa miguu ya   sensa katika Wilaya ya Rufiji ambapo ametoa seti 6 za jezi kwa timu sita na  mipira  12 kwa ajili ya mashindano  hayo.

Amesema lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha  wananchi  kushiriki kuhesabiwa  kwenye sensa ya kitaifa  yam waka huu  kwa manufaa mapana ya wananchi wa Rufiji na Taifa kwa ujumla

Aidha, amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Rufiji na watanzania wote kujitokeza kwa wingi Agosti 23, mwaka huu kuhesabiwa kwenye zoezi la sensa kitaifa.

Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya ya Rufiji amemshukuru Mhe. Mchengerwa  kwa jitihada  zake  na mchango wake kwenye sekta ya michezo ambapo amemhakikishia kuwa michango anayotoa itatumika vizuri ili  kupata matokeo chanya.


Post a Comment

Previous Post Next Post