Na. John Mapepele.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Rais Samia ameupiga mwingi hadi ameondoka nao kutokana na kuleta mapinduzi makubwa na mafanikio lukuki katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja ambapo amewataka wadau wote kuishi katika falsasa zake ili kuenzi kwa ufasaha maono na nia njema ya Mhe. Rais.
Kauli hiyo ameitoa leo Machi 29,2022 kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya mafanikio ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kipindi cha mwaka moja tangu aingie madarakani Machi 19 mwaka jana.
Amekemea vitendo vya baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakitumia nafasi walizonazo vibaya kwa kujinufaisha wenyewe au kuhujumu maendeleo ya michezo wanayoisimamia.
“Viongozi wenzangu niwaombe na kuwasihi sana tusimuangushe Mhe. Rais, bali Tuunge Mkono Juhudi zake, Nia njema na Uthubutu mkubwa aliounyesha katika kuleta mapinduzi kwenye sekta yetu na tuuenzi kwa vitendo.” Amefafanua, Mhe. Mchengerwa.
Amesema kama Waziri mwenye dhamana ya michezo hatafumbia macho wala kuvumilia Kiongozi yeyote wa sekta anazozisimamia kuanzia Wizarani, kwenye taasisi mpaka kwenye Vyama na mashirikisho ya michezo atakayefanya mambo ambayo hayakubaliki wakati Mhe. Rais amedhamiria kuvusha kwenye eneo hili.
Amesema anatambua wapo baadhi ya viongozi ambao kwa kipindi kirefu wanaendesha shughuli za vyama kwa mazoea bila kufuata taratibu wala kuheshimu na kutii mamlaka zinazosimamia Michezo, na amefafanua kuwa katika kipindi chake masuala ya Rushwa, Ubadhirifu wa mali na fedha za Umma, Upendeleo na Unyanyasaji katika Michezo hatayavumilia.
Ametaja baadhi ya mafanikio makubwa yaliyofanyika katika kipindi hiki kuwa ni pamoja na Ongezeko la bajeti,Uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, Ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya Kisasa ya michezo, kupitia Upya utekelezaji wa Sera ya Michezo ya Mwaka 1995, kuanzisha programu za kuibua vipaji vya michezo, ukarabati wa Uwanja wa Ndani wa Benjamini Mkapa, kutoa nafuu ya Kodi katika Uingizaji wa Nyasi bandia, kukamilika kwa uteuzi wa Shule 56 maalum za Michezo Nchini na ujenzi wa kituo Maalum cha maendeleo ya Michezo katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Mafanikio mengine ni ushiriki wa Mashindano ya kombe la Dunia timu ya mchezo wa Soka kwa Walemavu mwenzi Oktoba Nchini Uturuki na Michezo kwa Wanawake; Twiga Stars, Tanzanite, Serengeti Girls na Timu ya wanawake U19 ya KRIKETI.
Ametumia tukio hilo kutangaza uteuzi Kamati ya Hamasa kwa Michezo ya Jumuiya ya Madola na Kombe la Dunia kwa Watu wenye Ulemavu na Bodi tatu (3) za taasisi zilizo chini ya Wizara yake ambazo ni Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Bodi ya Filamu na Bodi ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambazo Bodi zake zilikuwa zimemaliza muda wake.
Pia amemthibitisha Bi. Neema Msitha kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Bi. Consolata Mushi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Riziki Juma Majala kuwa Msajili wa vyama vya Michezo nchini.
Katika kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa na wadau wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo. Dkt. Hassan Abbasi.