Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, akizungumza na wakazi wa Malampaka, Wilayani Maswa, kabla ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi ya kisasa ya SGR, sehemu ya Mwanza hadi Isaka (KM 349). Mkoani Simiyu na Mwanza
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akizungumza na wakazi wa Malampaka, Wilayani Maswa, kabla ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi ya kisasa ya SGR, sehemu ya Mwanza hadi Isaka(KM 349). Mkoani Simiyu na Mwanza.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho (wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa Meneja Mradi wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC-CRCC), Lu Haiqiang (aliyevaa kofia nyeupe) alipokagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi ya kisasa ya SGR, sehemu ya Mwanza hadi Isaka(KM 349).
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa maelekezo kwa Meneja Mradi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRC), Eng. Masanja Machibya (kulia) na China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC-CRCC), Lu Haiqiang (aliyevaa kofia nyeupe), alipokagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi ya kisasa ya SGR, sehemu ya Mwanza hadi Isaka(KM 349). Kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara.
************************************
Wananchi wa Malampaka, Wilayani Maswa, Mkoani Simiyu wameeleza faida za mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR Sehemu ya tano itakayojengwa kutoka Mwanza hadi Isaka KM 349 ikiwemo Upatikanaji wa ajira na ukuaji wa uchumi.
Akizungumza mbele ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, Mzee Juma Saidi amesema wako tayari kushiriki kwenye mradi na kuahidi kulinda vifaa vitakavyotumika kwenye ujenzi.
“Sisi tumeshajipanga kufanya kazi sababu tumeshaona vifaa vimewasili, tuko tayari kufanya kazi kwa bidii ili tupate kipato lakini pia tushiriki moja kwa moja kutimiza historia ya nchi kupitia mradi huu” amesema Mzee Saidi.
Kwa upande wake Waziri Dkt. Chamuriho amesema Serikali imeridhishwa na matayarisho ya mkandarasi kwani ameshaanisha maeneo ya kuweka kambi, eneo la kuchimba kokoto, kusilisha vifaa pamoja na kukamilisha reli ya mfano.
“Kama mnavyoona Mkadarasi yuko kwenye eneo la ujenzi na sehemu kubwa ya maandalizi imekamilika ikiwemo mitambo, hapa kitakachofata ni kumpa taarifa Mhe. Rais Samia Suluhu ili kuweka jiwe la msingi na ujenzi kuendelea” ameseama Waziri Chamuriho.
Waziri Chamuriho amesema Wizara itaendelea kusimamia kwa karibu miradi yote ya sekta ili ikamilike kwa ubora na wakati na kuwaomba wananchi kujipanga kutumia fursa hiyo kujiimarisha kiuchumi.
Aidha, Waziri Chamuriho amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda kwa kusimamia zoezi la kuhamasisha wananchi kupisha kwenye maeneo ambayo reli itapita na kuawaahidi wananchi hao kuwa uthamini utakapokamilika watalipwa fedha zako.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amewataka wananchi na wakazi wa Mwanza na Simiyu watakaopata kazi kwenye mradi huo kujiepusha na uwizi wa vifaa na mafuta ili kufanya mradi huo kukamilika kwa wakati.
“Katika sehemu nyingine kwenye ujenzi wa mradi huu kumetokea vitendo vya wizi sasa niwahakikishie Serikali haitamvumilia mwananchi yoyote atakayekamatwa na kifaa chochote kitakachokuwa kwenye mradi huu” amesisitiza Naibu Waziri Waitara.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza mradi huo mkubwa wa kitaifa na kumuahidi Waziri na Naibu Waziri kuwa wataimarisha ulinzi ili kufanikisha mradi huo.
Mradi huu wa ujenzi wa reli ya Kisasa unaanzia Dar es Salaam hadi Mwanza (KM 1219), umegawanyika katika sehemu tano ambazo ni Dar es Salaam mpaka Morogoro, Morogoro mpaka Makutupora, Makutupora hadi Tabora, Tabora hadi Isaka na sehemu ya tano ni Isaka mpaka Mwanza inayojengwa na kampuni ya China Civil Engineering Consruction Corporation (CCECC-CRCC) ambayo Mkataba wake ulisainiwa mwezi Januari mwaka huu.
Imetolewa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini