Watanzania Tudumishe Muungano” Waziri Ummy Mwalimu

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar Dkt. Khalid Mohammed mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Makamu wa Rais, Mtumba Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akionga kikao katika ya wataalamu wa Ofisi yake na ugeni kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar Dkt. Khalid Mohammed, mara baada ya kufanya ziara ya kujitambulisha.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar Dkt. Khalid Mohammed (wa pili kulia) mara baada ya kikao baina yao. Wengine katika picha ni Balozi Joseph Sokoine Kaimu Katibu Mkuu (wa pili kushoto), Balozi Mbarouk Mbarouk Mkurugenzi Idara ya Muungano na Khalid Hamrani Mkurugenzi Uratibu shughuli za Serikali – SMZ.

**********************************

Na Lulu Mussa

Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Ummy Mwalimu amezitaka Wizara ambazo zina hoja 11 za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kukaa mara moja ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.

Waziri Ummy ameyasema hayo hii leo katika kikao cha pamoja baina yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar Dkt. Khalid Mohammed mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.

Amesema tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha tunaimarisha Muungano wetu na kuhakikisha una kuwa imara kwasababu Muungano wetu ndio umoja wetu, usalama wetu na amani yetu.

“Hatutamvumilia mtu yoyote anayeleta chokochoko na kutaka kuvuruga umoja na mshikamano wa watanzania” Ummy alisisitiza.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dkt. Khalid Mohammed amesema Serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimefanya kazi kubwa katika kuondoa changamoto kumi ndani ya kipindi cha miaka mitano.

“Kupitia vikao vya Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ndani ya kipindi cha miaka mitano jumla ya changamoto 21 ziliwasilishwa na kati ya hizo changamoto 10 zimepatiwa ufumbuzi, ni imani yangu kuwa zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi kwa kuwa viongozi wetu wana dhamira ya dhati” amesisitiza Dkt. Khalid.

Amesema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar imeanza matayarisho ya ujenzi katika kiwanja chenye ukubwa wa ekari 33 katika eneo la Mahoma Makulu, Dodoma ili kurahisha kazi ya uratibu.

“Hakuna sababu ya sisi kubaki Dar es Salaam, tutahakikisha tunahamia Dodoma mapema  iwezekanavyo ili kufanya kazi kwa karibu”

Waziri Ummy amemuhakikishia Waziri Khalid kufanya kazi kwa pamoja  katika kuimarisha misingi ya amani, umoja na mshikamano kwa maslahi ya pande zote mbili za Muungano.

Post a Comment

Previous Post Next Post