TUMEZALISHA MBEGU BORA MILIONI 4 ZA MICHIKICHI ILI KUOKOA FEDHA ZA SERIKALI ZAIDI YA BILIONI 443 – KATIBU MKUU KUSAYA

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akijiandaa kuendesha trekta aina ya Holland TT75 (HP 75). Trekta alilokabidhi kwa Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Geoffrey Mkamilo ili litumike kwenye shughuli za maendeleo ya utafiti wa zao la chikichi, leo tarehe 17.12.2020 katika ziara yake katika Kituo mahiri cha utafiti wa zao hilo (TARI Kihinga) mkoani Kigoma.

Sehemu ya miche ya michikichi katika kitalu cha Kituo mahili cha zao la chikichi (TARI Kihinga).

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo kuhusu mifuko maalum ya kuoteshea miche bora ya michikichi, leo tarehe 17.12.2020 katika ziara yake katika Kituo mahiri cha utafiti wa zao hilo (TARI Kihinga) mkoani Kigoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo kuhusu maendeleo ya uzalishaji wa mbegu bora pamoja na miche ya michikichi leo tarehe 17.12.2020 katika ziara yake katika Kituo mahiri cha utafiti wa zao hilo (TARI Kihinga) mkoani Kigoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akifuatilia wasilisho pamoja na Watumishi wa TARI Kihinga kutoka kwa Msimamizi Kituo hicho, Dkt. Filson Kagimbo (Hayupo pichani). Leo tarehe 17.12.2020. Kulia kwa Katibu Mkuu ni Dkt. Geoffrey Mkamilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI).

**********************************

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya amesema Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo (TARI – Kihinga) imefanikiwa kuzalisha mbegu bora milioni 4 za zao la chikichi kama sehemu ya mkakati wa kuokoa fedha za Serikali wa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 443 ambazo zimekuwa zikitumika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Katibu Mkuu Kilimo Bwana Kusaya ameyasema hayo leo tarehe 17.12.2020 wakati wa ziara yake ya siku tatu ya kutembelea, kukagua na kujionea shughuli za maendeleo ya Sekta ya Kilimo mkoani Kigoma ambapo leo ametembelea Kituo mahiri cha utafiti wa zao la chikichi (TARI Kihinga) katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji.

Katibu Mkuu Kusaya amesema hadi kufikia tarehe 10 Desemba, 2020 Kituo cha TARI Kihinga kimezalisha zaidi ya mbegu bora 4,205,335 za zao la chikichi na zimetolewa kwa Halmashauri sita za mkoa wa Kigoma; Zinazolima zao hilo.

Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa ya Kigoma – Ujiji, Wilaya ya Kigoma, Wilaya ya Kasulu, Mji wa Kasulu, Wilaya ya Uvinza na Wilaya ya Buhigwe.

Katibu Mkuu Kusaya amesema mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 570,000 kila mwaka ambapo uwezo wa nchi kuzalisha ni tani 205,000 sawa na asilimia 36% na kuongeza kuwa kiasi cha tani 365,000 sawa na asilimia 64 ya mafuta huagizwa toka nje na kuigharimu nchi kiasi cha shilingi biloni 443 kila mwaka.

Katibu Mkuu Kusaya amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo Wizara iliona ni vyema kuanza na uzalishaji wa mbegu bora.

“Uwezi kukabiliana na changamoto ya namna hiyo bila ya kuanza na mbegu; Ndiyo maana tumeona tuanze na mbegu bora kwanza; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alitoa maelekezo ya kuondokana na utegemezi huo tarehe 28 Julai, 2018 baada ya kufanya kikao na Wadau ili kuweka mkakati wa upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kupitia uendelezaji wa zao la chikichi.”

“Mojawapo ya mkakati ni kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za michikichi zinazotoa mafuta mengi kuliko zinazolimwa sasa.” Amekaririwa Katibu Mkuu Kusaya.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa Serikali imeamua kuanza na mkoa wa Kigoma na kuongeza kuwa zaidi ya mikoa 16 imeonyesha kuwa na fursa ya kupanda zao la chikichi.

Katibu Mkuu Kusaya ametoa wito kwa Halmashauri sita za mkoa wa Kigoma kuendelea kuzalisha miche milioni moja kupitia mbegu bora hizo zilizozalishwa na kutolewa na Kituo cha TARI Kihinga na ameendelea kuhimiza ushirikiano katika ya Halmashauri hizo na Kituo hicho.

Katika Taarifa yake kwa Katibu Mkuu Kilimo Gerald Kusaya Msimamizi wa Kituo cha TARI Kihinga Dkt. Filson Kagimbo amesema hadi sasa kiasi cha mbegu 1,863,111 zilishatolewa kwa Taasisi nyingine za Umma na Sekta Binafsi.

Amezitaja Taasisi hizo ni pamoja na TARI Kihinga yenyewe (120,000), JKT Bulombora (219,691), Gereza la Kwitanga (286,125), Gereza la Ilagala (15,795), Shamba la Wakala wa Mbegu za Kilimo, ASA – Bugaga (50,000), Taasisi ya Utafiti Ilonga – TARI Ilonga (235,500) na Sekta Binafsi mbegu (936,000). Baada ya Taasisi hizo kupewa mbegu hizo ambapo jumla ya miche 1,087,143 imezalishwa.

Dkt. Kagimbo ameongeza kuwa Jumla ya Halmashauri sita za mkoa wa Kigoma zilipewa kiasi cha mbegu 306,000 ambapo jumla ya miche 183,175 ilizalishwa. Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa ya Kigoma – Ujiji, Wilaya ya Kigoma, Wilaya ya Kasulu, Mji wa Kasulu, Wilaya ya Uvinza na Wilaya ya Buhigwe.

Wakati huo huo katibu Mkuu Kusaya amekabidhi trekta kama sehemu ya kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mbegu bora pamoja na miche kwa kituo cha TARI Kihinga. Trekta hilo lenye thamani ya shilingi milioni 75 limekabidhiwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za Taasisi hiyo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa hadi sasa Jumla ya shilingi bilioni 1.4 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza zao la chikichi kupitia Kituo cha TARI Kihinga.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI Makao Makuu) Dkt. Geoffrey Makamilo amemshukuru Katibu Mkuu kupitia Wizara ya Kilimo kwa kutoa fedha kiasi cha Tsh 1,457,952,000 kwa ajili ya kuzalisha mbegu na kuimarisha miundo mbinu ya TARI Kihinga pamoja na ununuzi wa gari la Watumishi pamoja na ununuzi wa trekta hilo pamoja na zana zake.

Post a Comment

Previous Post Next Post