CHUO KIKUU CHA USHIRIKA MOSHI FANYENI TAFITI KUBORESHA UTENDAJI KAZI WA VYAMA VYA USHIRIKA – KM KUSAYA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( wa nne toka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi leo alipofanya ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kulia) akiwa kwenye mazungumzo na Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Dkt.Khatibu Kazungu (katikati) leo alipofika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kusaini kitabu cha wageni.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akitazama shamba la mpunga la chuo cha Mafunzo ya Kilimo  Kilimanjaro (KATC) leo alipofanya ziara ya kazi na kuongea na watumishi. Akiwa shambani hapo amekitaka chuo hicho kubuni miiradi ya kilimo ili kijiendeshe kibiashara hivy ameahidi kuwapatia trekta kubwa kwa ajili ya kilimo cha mpunga na kufundishia wanafunzi.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akisoma kitabu kwenye maktaba ya chuo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro ( KATC). Akiwa chuoni hapo amesema Wizara itaanzisha maabara ya kielektoniki ( e-Learning) ili kuboresha mafunzo kabla ya Desemba mwaka huu.

…………………………………………………………..

Wizara ya Kilimo imekitaka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) kuwa na utaratibu wa kufanya utafiti kujua namna ambavyo jamii ya watanzania inanufaika na ushirika nchini ili kiboreshe mitaala yake ya kufundishia.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ametoa rai hiyo leo alipozungumza na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi baada ya kukitembelea ikiwa ni sehemu ya ziara yake kukagua utendaji kazi wa taasisi zinazofanya kazi ya kuinua sekta ya kilimo nchini.

Amesema chuo hicho kina mchango mkubwa katika kuifanya sekta ya ushirika nchini kuchangia ukuaji wa uchumi na kuwezesha wana ushirikia kunufaika na kazi zao kupitia mafunzo yanayotolewa kwa wataalam.

“Nendeni kwenye vyama vya ushirika na AMCOS kuangalia namna wanavyotekeleza majukumu yao na kuwapa mafunzo ya kuboresha ili ushirika uwe na mchango katika kukuza kilimo na pato la wakulima” ameeleza  Kusaya

Kusaya amekitaka pia chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kuanzisha ushirikiano wa karibu na Tume ya Maendeleo ya Ushirika ( TCDC) pamoja na Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika ( COASCO) zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kufundisha wana ushirika wakiwemo watumishi ili sekta hiyo iweze kusaidia ushirika kuondokana na kero za ubadhirifu na usimamizi mbaya wa mali za wakulima.

Ili kufika lengo la kufanya watendaji wa vyama vya ushirika wawe na weledi na ujuzi Katibu Mkuu huyo ametoa wito kwa chuo kuanzisha utaratibu wa kuwapanguia wanafunzi wake kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye vyama vya ushirika na AMCOS kote nchini kuanzia mwaka huu.

“Wanafunzi wanosoma hapa tutawapa nafasi ya kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye vyama vyetu vya Ushirika ili wasaidie kuimarisha utendaji kazi wa ushirika hali itakayowapa pia watumishi wa vyama hivyo weledi “amesema  Katibu Mkuu Kusaya.

Katika hatua nyingine Kusaya alisema wizara yake inatekeleza agizo la Waziri Mkuu la kuhakiksha vyama vya ushirika vinaongozwa na watendaji wenye sifa na weledi wa ushirika ili kuondoa tatizo la ubadhirifu na utendaji mbovu ambapo kwa kuanzia wataajiliwa Mameneja Wakuu wa Vyama vikuu vya Nyanza ,Shirecu na KCU .

Akitoa taarifa ya chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof.Alfred Sife alisema chuo kimeendelea kuwa na mafanikio katika kufundisha taaluma ya ushirika nchini na wanafunzi wengi wamenufaika baada ya kuhitimu.

Ameeleza pia kazi kubwa chuo Kikuu cha ushirika Moshi inachokifanya ni kuzalisha rasilimali watu wanaoweza kuendesha vyama vya Ushirika na kushiriki katika uchumi wa nchi.

“ Chuo chetu kinazalisha wataalam wengi lakini ukienda katika vyama vya ushirika huko kwenye jamii huwakuti ndio maana utakuta taarifa nyingi za ukaguzi wa hesabu na mali za ushirika zinazotolewa na COASCO zinaonyesha uwepo wa tatizo la utunzaji hesabu” amesema  Prof.Sife

Prof Sife ameongeza kusema anaomba Wizara ya Kilimo ambayo kwa kiwango kikbwa ndio yenye vyama vya ushirika kutokana na sekta ya Kilimo kushirikiana na chuo kutoa mafunzo ya muda mufupi kwa watendaji na viongozi wa ushirika ili waweze kutekleza majukumu yao kwa weledi na kufanya ushirika wa kisayansi na kutumia teknolojia rahisi ikiwemo mfumo wa upatikanaji tawimu sahihi za wana ushirika na manufaa wanayopata
kiuchumi.

Kwa mujibu wa Makamu Mkuu huyo alisema chuo hicho katika mwaka wa masomo 2020/21 kina wanafunzi 7,231 waliopo kwenye program zaidi ya 36 zinazofundishwa chuoni hapo huku kikiwa na idadi ya watumishi 338 tangu kilipoanzishwa mwaka 2014 .

Awali Katibu Mkuu Kusaya alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Khatibu Kazungu kuhusu mwenendo na changamoto za sekta ya kilimo kwenye mkoa huo. Katibu Mkuu yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya kukagua uetendaji kazi wa taasisi chini ya wizara na kufanya ufuatiliaji wa viwanda vya kuzalisha mbolea nchini .

Post a Comment

Previous Post Next Post