
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI,Prof. Riziki Shemdoe, akizungumza na waandishi wa habari ( Hawapo Pichani ) jijini Dodoma Aprili 11, 2026 kuhusu nafasi ya wahitimu wa Kidato cha Nne 2025 kubadilisha machaguo ya tahasusi na kozi kwa mwaka wa masomo 2026.
Na. Mwandishi Wetu Dodoma,
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka 2025 kubadilisha machaguo ya tahasusi na kozi walizochagua kwa ajili ya kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo vya kati pamoja na elimu ya ufundi mwaka 2026.
Akizungumza na waandishi wa Habari Aprili 11,2026, Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa fursa hiyo inalenga kuwapa wanafunzi nafasi ya kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu walioupata katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).
Pia, Prof. Shemdoe Amesema kuwa serikali imekamilisha zoezi la kuingiza taarifa zote za wanafunzi kwenye kanzidata baada ya kukusanya taarifa kutoka kwenye fomu za uchaguzi (Selform) zilizojazwa wakiwa shuleni.
Aidha, amebainisha kuwa kukamilika kwa zoezi hilo kunawawezesha wanafunzi kufanya marekebisho ya machaguo yao kwa njia ya mtandao kupitia Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Student Selection MIS), ambapo taarifa hizo zitatumika katika kuwachagua na kuwapangia shule na vyuo kulingana na ufaulu na machaguo yao.
Pia ameongeza kuwa zoezi hilo linatoa nafasi kwa wanafunzi kuongeza au kubadilisha tahasusi na kozi ili kuwaandaa vyema kitaaluma kwa maisha yao ya baadaye.
Amesema kuwa zoezi hilo linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wanafunzi, wazazi na walezi, huku akisisitiza umuhimu wa kushauriana kikamilifu ili kufanya maamuzi sahihi ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu na malengo ya mwanafunzi.
Aidha, amebainisha kuwa wanafunzi wanatakiwa kuingia kwenye mfumo huo kwa kutumia namba yao ya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2025, jina la mwisho, mwaka wa kuzaliwa pamoja na taarifa nyingine zitakazohitajika na mfumo.
Ameongeza kuwa zoezi la kubadilisha tahasusi na kozi litaanza rasmi Aprili 11, 2026 hadi Mei 10, 2026, na kuhimiza matumizi sahihi ya muda huo ili kuepusha changamoto baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo.
Aidha, Ameeleza kuwa baada ya matokeo hayo kutangazwa, hakutakuwa na nafasi ya kushughulikia changamoto zitakazotokana na mabadiliko ya machaguo.
Prof. Shemdoe, ameongeza kuwa Huduma ya kubadilisha tahasusi ni bure, amewahimiza Wanafunzi na Wazazi kuwasiliana na Dawati la Huduma kwa Wateja la TAMISEMI kupitia barua pepe: huduma@tamisemi.go.tz au kuwasiliana moja kwa moja na Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa simu +255 262 160 210 na +255 735 160 210 au kufika katika ofisi za elimu za mikoa na halmashauri endapo watakumbana na changamoto wakati wa zoezi hilo.