MWANDISHI NGULI ABDILATIF ABDALLA AWASILI KWA TUZO YA MWALIMU NYERERE YA UANDISHI BUNIFU


 Mwandishi nguli wa vitabu na mshairi, Abdilatif Abdalla, ambaye ni mgeni rasmi katika hafla ya Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu itakayofanyika kesho, Aprili 13, 2026, amewasili nchini na kueleza kuwa ni heshima kubwa kwake kupewa hadhi hiyo.

Akizungumza leo Aprili 12, 2026 mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Abdalla amesema anajivunia kutambuliwa na kupewa nafasi ya kushiriki katika tuzo hizo muhimu kwa maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

“Hii ni heshima kubwa kwangu kama mwandishi kupata hadhi hii ya kuwa mgeni rasmi katika tuzo zinazotambua mchango wa Hayati Nyerere katika kukuza Kiswahili duniani kote,” amesema Abdalla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Penina Mlama, ameonesha kufurahishwa na ujio wa mgeni rasmi huyo, akieleza kuwa ni fahari kwa waandishi bunifu nchini kuwa na kiongozi anayeshiriki taaluma hiyo hiyo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) amewakaribisha wageni wote kushiriki katika hafla hiyo, akisisitiza kuwa tuzo hizo zina lengo la kuendeleza uandishi bunifu na kuhamasisha utamaduni wa kusoma vitabu nchini.

Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu hufanyika kila mwaka Aprili 13, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere.       

Post a Comment

Previous Post Next Post