KASULU YAZIDI KUNUFAIKA NA MALIASILI NA UTALII

 Na Sixmund Begashe, Dodoma


Wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini wameendelea kunufaika na uwepo wa mwekezaji katika kitalu cha Makere Forest Reserve kwa kupata mgao wa fedha za maendeleo ya jamii zaidi ya Shilingi Milioni 12 kila mwaka kinacholipwa na mwekezaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya vijiji.

Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Edibil Kazala Kinyoma alipotaka kujua "Je, ni kwa kiasi gani wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini wananufaika na uwepo wa Mwekezaji wa kitalu cha Makere Forest Reserve".

Dkt. Kijaji amesema kuwa kwa kuzingatia vipaumbele vya vijiji husika katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 Vijiji vya Kagera Nkanda, Chekenya na Kabulanzwili vililipwa Shilingi 4,356,435.67 kila kimoja.

"Vilevile, mgao wa fedha zinazotokana na asilimia 25 ya ada ya wanyamapori wanaowindwa katika kitalu husika kwa mujibu wa Kifungu cha 137 cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2025 zinalipwa na Serikali kwa Halmashauri husika". Alifafanua Dkt. Kijaji

Ameongeza kuwa asilimia 60 ya fedha hizo hutumika kutekeleza miradi ya maendeleo na asilimia 40 shughuli za uhifadhi katika vijiji vinavyozunguka kitalu husika.

"Sambamba na manufaa yaliyotajwa, katika kipindi cha mwaka 2024/25 na 2025/26 mwekezaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) wamechangia miradi ya jamii yenye thamani ya shilingi 166,475,000". Aliongeza Dkt. Kijaji

Aidha, Dkt. Kijaji amesema kuwa fedha hizo zimetumika kufadhili kambi ya huduma ya matibabu ya macho katika Halmashauri ya Kasulu, madawati 100 katika Shule za Msingi Chekenya (25), Nyakasanda (25) na Nyantuku (50) na uchimbaji wa visima vya maji sita (6) katika Shule za Msingi Kamganza, Kasasa, Mwitiri, Chekenya na Nyantuki pamoja na Kituo cha Afya cha Kagerankanda.


Post a Comment

Previous Post Next Post