Mwandishi Wetu,
Serikali imesema imefanikiwa kuimarisha sekta ya kilimo nchini, ambapo uzalishaji wa chakula umefikia kiwango kinachokidhi mahitaji ya taifa kwa zaidi ya asilimia 130, hatua inayotajwa kuwa ni mafanikio makubwa katika kuhakikisha usalama wa chakula.
Akiwasilisha bungeni jana, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba alisema uzalishaji wa mazao umefikia tani 23,783,128 katika msimu wa mwaka 2024/2025, ukilinganishwa na mahitaji ya tani 18,279,054 kwa mwaka 2025/2026.
Alimnukuu Julius Kambarage Nyerere akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli huanza pale wananchi wanapoweza kuzalisha chakula cha kuwatosha wenyewe, akieleza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira bora ya kufanikisha azma hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na upatikanaji wa pembejeo kwa wakati pamoja na utoaji wa ruzuku ya mbolea. Alieleza kuwa katika msimu wa 2025/2026, Serikali imetoa tani 1,098,990 za mbolea, sawa na asilimia 73.26 ya lengo lililowekwa.
Kati ya hizo, tani 574,664.99 zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.03 zimesambazwa kwa wakulima 526,044 kupitia mpango wa ruzuku, hatua iliyochochea ongezeko la matumizi ya mbolea na kuongeza tija shambani.
Takwimu zinaonesha kuwa, matumizi ya mbolea yameongezeka kwa asilimia 14.6, kutoka tani 848,884 mwaka 2023/2024 hadi tani 972,506 mwaka 2024/2025.
Aidha, matumizi ya virutubisho yamepanda kutoka kilogramu 19 hadi 24 kwa hekta.
