MKENDA: TUZO YA MWALIMU NYERERE KUENDELEZA KISWAHILI, ORODHA TEULE YATAJWA


 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kuhusu tuzo ya Uandishi Bunifu ya Mwalimu Julius Nyerere itakayofayika Aprili 13, 2026 jijini Dar es Salaam. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hiyo, Profesa Penina Mlama akifafanua jambo kuhusu tuzo hiyo. 

Naibu Waziri  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wanu Hafidh Ameir akizungumza jambo katika kikao hicho. 

………..,. 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ametangaza kufanyika kwa hafla ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu 2026, akisema tuzo hiyo ni nyenzo muhimu ya kukuza lugha ya Kiswahili na kuibua vipaji vya waandishi nchini.

Akizungumza  Kikao kilichofanyika ofisi ya wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia jijini dodoma , Prof. Mkenda amesema, “tumewaita leo ili kuendelea kuhakikisha umma wa Watanzania unapata taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya sekta ya elimu, hususan kupitia Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, ambayo inalenga kukuza fasihi na ubunifu wa Watanzania.”

Ameongeza kuwa utoaji wa tuzo hiyo hufanyika kila Aprili 13, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, akisema, “tunaenzi mchango wake mkubwa katika kukuza lugha ya Kiswahili, utamaduni na tunu za Taifa letu.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hiyo, Profesa Penina Mlama, amesema mchakato wa tuzo hiyo umefanyika kwa mwaka mzima ukihusisha upokeaji na uchambuzi wa miswada kutoka kwa washiriki mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Hadi sasa majaji wamekamilisha kazi ya kusoma miswada yote iliyowasilishwa na tumepata orodha teule ya washiriki watakaoingia hatua ya mwisho ya kuwania tuzo. Majina haya yamepangwa kwa alfabeti na si kwa kuonyesha mshindi,” amesema Prof. Mlama.

Amefafanua kuwa kwa mwaka 2026, tuzo hiyo inahusisha vipengele vinne ambavyo ni riwaya, ushairi, hadithi za watoto na tamthiliya, huku washindi watatu bora kwa kila kipengele wakitarajiwa kutangazwa rasmi katika hafla itakayofanyika Aprili 13, 2026, jijini Dar es Salaam.

Katika kipengele cha riwaya, walioteuliwa ni Abbas Mohamed Omar, Ahmad Simba Mwaita, Bishop John Hiluka, Dotto Rangimoto, Emmanuel Felix Chifunda, Enock Abiud Maregesi, Gabriel Amanti Shewio, Halfani Sudy, Hussein Msafiri Wamaywa na Nickson Elia Mbala Chozi.

Kwa upande wa ushairi, majina yaliyotajwa ni Abdallah Salim Ngereza, Ali Omar Mansour, Amri Rajabu Abdalah, Hafidh Ali Makame, Hassani Mbwana Mzuka, John Kumbulwa Joseph, Kombo Abdallah Omar, Matina Nseka Mbilibili, Mbonea Jasper Berya na Ramadhani Halidi Ally, wakiwa na miswada mbalimbali ikiwemo “Urithi wa Lulu”, “Waraka Kutoka Gerezani” na “Tunu ya Taifa.”

Katika hadithi za watoto, waliopendekezwa ni Amina Abdulrahman Mohammed, Amnah Feisal-Amin Ibun, Christopher Zacharia Lameck, Cloud Augustino Chatanda, Fatuma Salim Suleiman, Godlove Kabati Selestine, Istiqamah Ahmed Mbwana, Mwanacha Mohamed Omar, Naomi William Jasseda na Tune Shaaban Salim.

Aidha, kwa upande wa tamthiliya, walioteuliwa ni Elizabeth Godwin Mahenge, Esther Evarist Nyawale na Hamisi Hussein Kibari kupitia kazi zao “Fanani”, “Jiko la Ukombozi” na “Ufalme wa Mabadiliko.”

Prof. Mkenda amesisitiza dhamira ya serikali kuendeleza tuzo hiyo akisema, “tutaendelea kuwekeza katika uandishi bunifu kwa kuwa ni sehemu muhimu ya kujenga utamaduni wa kusoma, kuhifadhi historia na kukuza sekta ya uchapishaji vitabu nchini.”

Naye Prof. Mlama ameongeza kuwa mwitikio wa washiriki umekuwa mkubwa na unaonyesha kukua kwa tasnia ya uandishi bunifu, akibainisha kuwa washindi watatu bora kwa kila kipengele watapata zawadi ya fedha taslimu pamoja na fursa ya kuchapishiwa kazi zao.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo inatarajiwa kufanyika Aprili 13, 2026 katika ukumbi wa Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam, ikiwakutanisha wadau wa fasihi, waandishi na wapenzi wa lugha ya Kiswahili kutoka ndani na nje ya nchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post