TEMESA YAKAMILISHA UKARABATI WA MV KAZI

 NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV


WAKALA wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), imekamilisha matengenezo ya kivuko cha MV Kazi ambacho kilileta hitirafu mwanzoni mwa mwezi huu, kinatarajiwa kuanza kazi hapo kesho Januari 13, 2026 mchana.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Kaimu Mtendaji Mkuu TEMESA, Mosses Mabamba, amesema ukarabati wa kivuko hicho umechukua siku nne na kugharimu jumla ya shilingi milioni 30.

Ameeleza kuwa kazi hiyo imelenga kuhakikisha usalama na ufanisi wa huduma kwa wananchi wanaotegemea kivuko hicho.

"Majaribio ya kivuko hiki (MV Kazi) yatafanyika kesho asubuhi, na kuanzia majira ya saa nane mchana, kitaanza rasmi kutoa huduma kwa wananchi wa eneo la Feri na Kigamboni na kuweza kupunguza changamoto". Amesema

Aidha, Mabamba amebainisha kuwa kwa sasa kivuko cha MV Kazi kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 20 kwa safari moja, hatua inayolenga kupunguza msongamano na kurejesha hali ya kawaida ya usafiri katika eneo hilo.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wanaotumia kivuko hicho wamesema kurejea kwa huduma ya MV Kazi ni faraja kubwa kwani itarahisisha shughuli zao za kila siku, ikiwemo kwenda kazini, shuleni na katika shughuli za kibiashara.

Hata hivyo, wameitaka Serikali kuendelea kuboresha huduma za vivuko ili kuepuka adha zinazojirudia.

Wakati huo huo, Serikali imeweka mpango wa muda mrefu wa kuboresha usafiri wa majini kwa kuendelea na ukarabati wa kivuko cha MV Magogoni, kinachotarajiwa kuanza kutoa huduma mwezi Aprili.

Kivuko hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 2,000 na magari 60 kwa safari moja, hatua inayotajwa kuonesha dhamira ya Serikali katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa majini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama, ya uhakika na endelevu.



Post a Comment

Previous Post Next Post