Na WAF, DODOMA
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema, Serikali imechukua hatua madhubuti za kuhakikisha wazee na watoto wanapata huduma za matibabu bila vikwazo ya kifedha kupitia Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Conchesta Leonce Rwamlaza, aliyehoji ni lini Serikali itatunga sheria maalum ya kulinda utoaji wa huduma za matibabu bure kwa wazee na watoto, Dkt. Mollel amelimbia Bunge kuwa, sheria hiyo tayari imetungwa na imeyagusa makundi maalum, wakiwepo wanawake wajawazito na watoto walio chini ya miaka mitano, yanapata huduma za afya bila malipo.
“Kutekelezwa kwa Sheria hii kutatoa uhakika wa upatikanaji wa huduma za matibabu kwa makundi yote yenye uhitaji, bila kujali hali zao za kiuchumi,” amesema Dkt. Mollel.
Sheria hiyo imeanzisha mfuko maalum wa kuhudumia watu wasio na uwezo, ikiwa ni hatua muhimu za kuboresha huduma za afya na kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bila kikwazo cha fedha.