WALIPAKODI MKOANI TABORA WAAHIDI USHIRIKIANO NA TRA

 Walipakodi mkoani Tabora wameahidi kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kulipa Kodi kwa hiari na kuwafichua Wafanyabiashara wanaokwepa Kodi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano baina yao na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda Wafanyabiashara hao wamesema wanajivunia kulipa Kodi kutokana na maendeleo makubwa yanayofanywa na serikali.

Alex Mlifwe, Isihaka Yange na Shaban Muhinda ni miongoni mwa Wafanyabiashara waliozungumza kwenye mkutano huo na kuiomba TRA kuwafikia Walipakodi wengi zaidi hasa waliopo katika maeneo ya vijijini.

Wamesema wapo watu wengi wanaofanya biashara bila kulipa Kodi Hali inayowaumiza wachache wanaolipa Kodi maana masoko wanayotumia ni ya aina moja na kushari wote wafikiwe.

Akizungumza na Wafanyabiashara hao pamoja na kujibu baadhi ya hoja za Wafanyabiashara Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amewashukuru Walipakodi mkoani Tabora kwa kuendelea kuiunga mkono TRA kwa kulipa Kodi kwa hiari.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema kama ilivyo katika maeneo mengine amekutana na Wafanyabiashara hao kwa lengo la kuwashukuru na kusikiliza changamoto zao pia kuzipatia ufumbuzi ili kuweka mazingira rafiki katika ukusanyaji wa Kodi.

Amesema Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan alimuagiza wakati akimuapisha kuwa asimamie ukusanyaji wa Kodi bila kutumia nguvu na ndicho anachokisimamia hali ambayo imeongeza makusanyo ya Kodi na kufanya TRA ivuke malengo ya makusanyo kwa kipindi cha miezi 7 mfululizo.

Kuhusu watu wanaokwepa Kodi amewaomba Wafanyabiashara hao kushirikiana na TRA kuwafichua ili idadi ya walipakodi nchini iongezeke hali inayoweza kupunguza viwango vya Kodi.

Kuhusu suala la Elimu kwa Mlipakodi Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA inaendelea kutoa elimu ili kuwezesha walipakodi kutambua wajibu wao na kujua walipe kiasi gani, walipe muda gani na kwa namna gani.








Post a Comment

Previous Post Next Post