UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU WACHAGIZA ONGEZEKO LA WAGENI SAADANI

 

Na. Edmund Salaho – Saadani.

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji leo tarehe 01, Februari 2025 ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuboresha miundombinu ikiwemo Barabara ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia ongezeko la wageni katika Hifadhi ya Taifa Saadani.

Kamishna Kuji ameyasema hayo wakati wa Kikao kazi kilichofanyika katika Hifadhi ya Taifa Saadani lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi wa Maafisa na Askari wa Hifadhi hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Nimepokea Taarifa ya Saadani kuna ongezeko la watalii zaidi ya asilimia kumi na saba mafanikio haya yamepelekea kuongezeka kwa mapato kufikia billioni 1.7 ikiwa ni makusanyo ya miezi saba huku makadirio yakiwa ni billioni mbili kwa mwaka katika Hifadhi hii ni jambo la kupongeza sana kila mmoja wetu Afisa kwa Askari amechangia mafanikio haya na TANAPA tumejipanga kutoka kwenye kukusanya billioni na kwa sasa tunaenda kwenye Trillioni”

“Mafanikio haya ya TANAPA ni matokeo ya mchango wa kila hifadhi ili kufikia lengo kuu la Serikali katika kuhifadhi na kuongeza mapato” alisema Kamishna Kuji.

Awali, akisoma Taarifa ya Maendeleo ya Hifadhi Afisa Uhifadhi Mkuu Glady’s Ng’umbi ambaye ni Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Saadani alibainisha kuwa maboresho makubwa ya miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Saadani yamechangia katika kuongezeka kwa watalii Saadani.

Akiyataja maboresho hayo ni pamoja na kuongezwa urefu kwa uwanja wa ndege Saadani kufikia urefu wa km 1.4 kutoka km 1.0 na ukarabati wa miundombinu ya barabara za utalii zilizopo zenye urefu wa Kilomita 74 na kufungua barabara mpya zenye urefu wa Kilomita 6.5.


Aidha, Ng’umbi alibainisha kuwa Hifadhi ya Taifa Saadani imejipanga kushirikiana na Taasisi nyingine ikiwemo Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kuongeza idadi ya watalii hifadhini kwa kutumia njia ya reli ya kutoka Dar mpaka Arusha na kuongeza kuwa tayari Hifadhi ya Taifa Saadani imeshafanya upembuzi yakinifu wa eneo la ujenzi wa gati (maegesho ya boti) ya kushushia wageni wanaotoka Zanzibar na Tanga kwa njia ya boti
na kutoa rai kwa wawekezaji kuchangamkia fursa za uwekezaji katika mazao mengine ya utalii wa kwenye maji (Blue Tourism).     

Post a Comment

Previous Post Next Post