WAZIRI DKT. PINDI CHANA AZINDUA TAKWIMU ZA WATALII NA MAPATO 2024


 Na John Bukuku, Dar es Salaam, Tanzania 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya utangazaji wa takwimu za watalii na mapato yatokanayo na utalii kwa mwaka 2024, amezindua rasmi taarifa hizo katika hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotangazwa, jumla ya watalii waliotembelea Tanzania kwa mwaka 2024 walifikia 5,360,247, ambapo watalii wa ndani walikuwa 3,218,352, na watalii wa nje walikuwa 2,141,895. Mapato yaliyopatikana kutoka sekta ya utalii kwa mwaka huo ni takribani Tsh trilioni 4.

Hata hivyo, mapato haya bado yako chini ya malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo inalenga kufikisha mapato ya Dola za Marekani bilioni 6 ifikapo Desemba 2025. Kwa sasa, sekta ya utalii inahitaji kuongeza mapato kwa zaidi ya Dola bilioni 2 ili kufikia lengo hilo.

Katika hotuba yake, Waziri Dkt. Pindi Chana alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya utalii kupitia filamu ya Tanzania: The Royal Tour, ambayo imechangia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi. Alieleza kuwa ushiriki wa Rais katika filamu hiyo umesaidia kuitangaza Tanzania kimataifa na kuimarisha taswira yake kama kivutio bora cha utalii.

Aidha, Waziri aliwapongeza viongozi na watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kujitoa kwao katika kusimamia sekta hiyo kwa bidii na ubunifu, akiwataka kuendelea kushirikiana na wadau wa utalii ili kuhakikisha sekta hiyo inazidi kuimarika.

Naye Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Nassoro Juma Kuji, alichangia mdahalo katika hafla hiyo, akieleza jinsi sekta ya utalii ilivyoimarika baada ya changamoto za janga la COVID-19. Alibainisha kuwa wakati wa janga hilo, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lilirekodi idadi ndogo sana ya wageni wa nje, hali iliyosababisha mapato kushuka hadi kufikia Tsh bilioni 57.

Hata hivyo, kupitia filamu ya Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania, aliyoifanya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mapato ya TANAPA yaliongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia Tsh bilioni 411 kwa mwaka wa fedha 2023/24. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/25, TANAPA imekusanya zaidi ya asilimia 80 ya mapato iliyopangiwa, ikiwa ni ndani ya miezi saba tu ya makusanyo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, wakiwemo wawakilishi wa makampuni ya utalii, wawekezaji, na viongozi wa mashirika yanayohusika na maendeleo ya sekta hiyo.

Katika hotuba yake, Waziri Dkt. Pindi Chana alisisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania, kuboresha miundombinu ya sekta hiyo, na kuendelea kushirikiana na wadau ili kuhakikisha utalii unakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa taifa.

        

Post a Comment

Previous Post Next Post