TANAPA YAWAALIKA WAGENI WA MKUTANO WA NISHATI KUTEMBELEA HIFADHI ZA TAIFA


Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Jully Lyimo.
                  ........................

 SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limesema lina matumaini kuwa wageni watakaoshiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, utakaofanyika Januari 27 na 28 jijini Dar es Salaam, watapata fursa ya kutembelea na kufahamu vivutio vya kipekee vilivyopo kwenye Hifadhi za Taifa nchini.

Akizungumza leo, Kamishna Msaidizi wa TANAPA, Bi. Jully Lyimo, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara wa shirika hilo, alisema TANAPA imejipanga vyema kutangaza utalii wa hifadhi kupitia mkutano huo unaotarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

“Tanzania inajivunia kuwa na hifadhi maarufu zenye vivutio vya kipekee ambavyo havipatikani Afrika wala duniani zaidi ya hapa nchini. Tunaamini kuwa kupitia mkutano huu, wageni watapata nafasi ya kufahamu na kutembelea hifadhi zetu,” alisema Bi. Lyimo.

Aliongeza kuwa TANAPA itakuwa na banda maalumu katika mkutano huo ambapo watatoa taarifa mbalimbali kuhusu vivutio vya hifadhi na mipango ya utalii kwa wageni na washiriki.

“Tunazo hifadhi zilizo karibu na jiji la Dar es Salaam kama Hifadhi ya Saadani, Hifadhi ya Mikumi na Hifadhi ya Milima ya Udzungwa ambazo wageni wanaweza kuzitembelea baada ya mkutano. Pia tuna Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mlima Kilimanjaro, na hifadhi zingine ambazo zina upekee wa aina yake,” aliongeza.

Aidha, Bi. Lyimo alisisitiza kuwa mikutano ya kimataifa kama huu inachangia kukuza utalii wa mikutano, ambao umekuwa kichocheo cha kuongezeka kwa idadi ya wageni wanaotembelea nchi na hifadhi mbalimbali za Tanzania.

“Tunatarajia wageni wengi zaidi kupitia utalii wa mikutano. Hii ni fursa ya wageni kupanga safari za baadaye pamoja na familia na marafiki kutembelea hifadhi zetu,” alihitimisha.

Post a Comment

Previous Post Next Post