SERIKALI IKO TAYARI KUSHIRIKIANA NA WADAU MAPAMBANO DHIDI YA MARBURG - DKT MAGEMBE

 


NA WAF, KAGERA

MGANGA Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe ameshukuru kwa utayari  ambao wameuonesha Wadau Sekta ya Afya katika kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg ambao umeripotiwa katika Wilaya ya Biharamulo, Kagera.


Ametoa shukurani hizo Januari 25, 2025 mara baada ya kuhitimisha ziara ya pamoja na wadau hao katika Maabara tembezi ya Afya ya Jamii iliyopo katika Kituo cha afya cha Kabyaile, Wilaya ya Misenyi.


Ameongeza kuwa suala la kukabiliana na ugonjwa huo linahitaji uratibu mzuri ili kutoleta changamoto, na ndio maana Serikali imewasikisha mkakati wa kukabiliana na ugonjwa huo kwa  wadau ukianisha maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau.


Pia ameyataja maeneo muhimu yaliyoainishwa katika mkakati huo ambayo yanahitaji rasilimali ni pamoja na utafiti,udhibiti, maabara jongezi, vifaa vya kuoshea mikono kwenye maeneo yenye mkusanyiko kama masoko na shule,  usafiri, uratibu, tiba, udhibiti mipakani pamoja na elimu ya afya huku akibainisha kwamba serikali tayari imeshatumia takribani bilioni 1 ambayo imeanza kuzaa matunda katika udhibiti wa ugonjwa huo. 


“Lengo letu ni moja, tuweze kupambana na ugonjwa huu na kuutokomoza, hivyo tutoe ushirikiano kwa kuchagua eneo ambalo mtashirikiana na Serikali” nasi tunaahidi kuwa misaada hiyo itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa” amefafanua Dkt. Magembe.


Awali Meneja wa Matukio ya Dharura na Majanga kutoka  Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Dkt. Dick Chamla amepongeza jitihada zilizofanywa na Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo ambapo amesema Serikali ya Tanzania imekuwa ya mfano kuanza kutumia rasilimali zake badala ya kusubiri wadau, na amesisitiza ushirikishwaji zaidi wa wadau katika kukabiliana  na ugonjwa huo. 


Wadau  wa Sekta ya Afya walioambatana na Mganga Mkuu wa Serikali kujionea hali halisi  ni pamoja na Shirika la Afya Duniani(WHO), MDH, Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), Kituo cha kudhibiti na kupambana na magojwa (CDC)Tanzania na Shirika la kimataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) naTaasisi ya Benjamin Mkapa.



Post a Comment

Previous Post Next Post