Mwandishi Wetu,
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaandaa utaratibu madhubuti wa kuhakikisha kuwa wazee wanahakiki taarifa zao za Bima ya Afya (NHIF) mahali walipo, bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NHIF kwa ajili ya kuhakikiwa.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma, Februari 7, 2025 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Mhe. Edward Ole Lekaita, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaweka mpango wa kuwafikia wazee kwa ajili ya uhakiki wa taarifa zao za Bima ya Afya ya (NHIF).
"Wazee hawatalazimika kusafiri tena ili kuhakiki taarifa zao, tumewaagiza wataalam waende moja kwa moja kwao ili kuwahudumia huko walipo," amesema Dkt. Mollel.