MOI YAANZA RASMI KUFANYA UPASUAJI WA UTI WA MGONGO KWA NJIA YA MATUNDU

 


Na Abdallah Nassoro-MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeanza rasmi kutoa huduma mpya za upasuaji uti wa mgongo kwa kutumia matundu (Spine Endoscope), kuanza kutolewa kwa huduma hiyo kutasaidia ufanisi wa upasuaji huo na kuwezesha wagonjwa kukaa siku cheche wodini.

MOI inakuwa taasisi ya kwanza nchini kutoa huduma hizo baada ya kupokea  mashine ya kisasa (Endoscope tower) ya kufanyia upasuaji huo yenye thamani ya Tsh. 500 Milioni kutoka kampuni ya Joimax ya nchini Ujerumani na kuifanya Taasisi ya MOI kuwa kinara katika utoaji wa huduma za upasuaji wa uti wa mgongo kwa matundu katika ukanda wa Afrika mashariki , kati na kusini  na kuchagiza dhana ya tiba utalii.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amebainisha hayo leo Februari, 5, 2025 wakati wa kambi maalum ya matibabu ya kibingwa ya uti wa mgongo kwa njia ya matundu ambapo wagonjwa 12 watafanyiwa upasuaji.

“MOI imekuwa Taasisi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuwa na kifaa hiki cha kisasa cha upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu...ufanisi wa upasuaji utaongezeka na wagonjwa watapona kwa haraka na kupunguza muda wa kukaa wodini” amesema Dkt. Mpoki

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo na Uti wa mgongo Dkt. Lemeri Mchome amesema huduma hiyo itasaidia wagonjwa kupata nafuu kwa haraka kutokana na kupata jeraha ndogo wakati wa upasuaji.

"Awali Taasisi ya MOI ilikuwa ikifanya upasuaji kwa kwa kufungua eneo kubwa hivyo kumlazimu mgonjwa kukaa muda mwingi wodini akiuguza jeraha na kumuacha na kovu kubwa... mgonjwa alikuwa analazwa siku tano au zaidi baada ya upasuaji kutokana na ukubwa wa jeraha, pia maumivu kwa mgonjwa yalikuwa makali, lakini kwa kutumia mashine hii changamoto hizo zote zitakuwa zimeisha " amesema Dkt. Lemeri

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Weill Cornel cha nchini Marekani Dkt. Osama Nazar Kashlan ameipongeza Taaisis ya MOI kwa kuwa tayari kuwekeza katika ujuzi wa watumishi wake na kuahidi kuendelea kuwajengea uwezo katika  huduma za kibingwa na kibobezi ili waendane na mabadiliko ya teknolojia duaniani.









Post a Comment

Previous Post Next Post