BARAZA LA WAFANYAKAZI BRELA LAZINDULIWA MKOANI MOROGORO

 


Godfrey Nyaisa, Ofisa Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) akizungumza  na wajumbe wa Baraza kwenye ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi na kikao cha  kwanza cha Baraza hilo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 mkoani Morogoro.

NA MWANDISHI WETU, MOROGORO

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), leo Februari 6, 2025 mkoani MOROGORO, imezindua Baraza la Wafanyakazi na kufanya kikao cha Kwanza kwa mwaka wa Fedha 2024/2025.
 
Katika uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la hilo, Godfrey Nyaisa amewakumbusha Wajumbe kutekeleza majukumu yao ili kuleta tija na ufanisi mahali pa kazi. 

Nyaisa alisema, “Baraza hili la Wafanyakazi wa BRELA lina jukumu la kipekee la kuchangia katika kuweka mazingira bora ya kazi yenye kuongeza tija, ushirikiano na maendeleo ya wafanyakazi, ambayo ndio uti wa mgongo wa mafanikio ya Taasisi.

 "Tunapokutana hapa ni fursa ya kutafakari mafanikio, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja kwa mustakabali wa Taasisi yetu.”   

Ameongeza kuwa Baraza la Wafanyakazi litakuwa na jukumu la kuishauri wakala kuhusu masuala yanayohusu maslahi ya watumishi, utekelezaji wa mipango na makisio ya mapato na matumizi ya Wakala, kupokea taarifa ya utekelezaji wa 
wakala na kutoa ushauri, kudumisha  ushirikiano kati ya watumishi na wakala katika uendeshaji wa Wakala na kushauri kuhusu ustawi wa wakala na maendeleo ya watumishi.  

Amesema kuwa pamoja na uzinduzi wa baraza hilo litafanya tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Taasisi kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kuangalia malengo yaliyopangwa, 
utekelezaji wa majukumu, changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, mikakati ya kukabiliana na changamoto husika. 

Pia amesema kuwa baraza litajadili na kupitisha makadirio ya Bajeti ya 
Wakala kwa mwaka wa fedha 2025/2026.  

Katika ufunguzi wa baraza hilo, pia lilifanya uchaguzi ambapo Peter Riwa, Ofisa Leseni Mwandamizi alichaguliwa 
kuwa Katibu na Gift Wazingwa, Ofisa Usajili alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi.

Mchakato huo wa ufunguzi na uchaguzi ulishuhudiwa na Brendan Maro, Dkt. Hussein Mugyabuso kutoka Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) na Christina Matage kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.  


Christina Matage Ofisa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,  Vijana, Ajira na watu wenye Ulemavu akitoa mafunzo juu ya namna ya uendeshaji  wa mabaraza ya wafanyakazi kwa  wajumbe wapya wa baraza la wafanyakazi kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) mkoani Morogoro.


Post a Comment

Previous Post Next Post