Chato, Geita Tanzania
Dkt. Diallo amewasihi wakulima wa pamba kununua mbolea pindi wanapouza mazao yao ili kuwawezesha kuzitumia wakati msimu wa kilimo unapowadia.
Amesema ni vyema wakulima kuhifadhi pembejeo badala ya fedha, kwani mahitaji ya kila siku ni mengi, na mara nyingi wakulima huishia kutumia fedha walizotenga kwa pembejeo, hivyo kulima bila kuitumia pembejeo hiyo muhimu.
Hayo yamebainika tarehe 18 Februari, 2025 wakati wa ziara ya Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Anthony Diallo katika vijiji vya Necezi na Songambele wilayani Chato.
Akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Necezi, Dkt. Diallo amesema ziara hiyo imelenga kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku na uhamasishaji unaofanywa na Mamlaka katika kuhamasisha matumizi sahihi ya Mbolea kwa wakulima wa zao la pamba na kujionea namna wanavyonufaika na mbolea hiyo.
“Tunataka kuhakikisha ruzuku inatumiwa ipasavyo. Maafisa ugani wamewapa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, na tumeona mafanikio. Tunataka wakulima wengine waige mfano wenu,” amesema Dkt Diallo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, amesema Mamlaka imeendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima kwa kuweka bei elekezi inayozingatia umbali wa Kijiji kilipo ili kuongeza motisha kwa wafanyabiashara lakini pia kuhakikisha mkulima ananunua pembejeo hiyo karibu eneo lake na kuongeza mwamko wa matumizi ya pembejeo hiyo.
“Awali matumizi ya mbolea yalikuwa kiasi cha tani 363,599 kwa mwaka 2021/2022 kutokana na bei ya pembejeo hiyo kuwa juu na kuwafanya wakulima kushindwa kumudu, lakini sasa tunatarajia kufikia matumizi ya tani milioni moja kwa msimu huu wa kilimo kwani wakulima wengi wameona tija inayotokana na matumizi sahihi ya mbolea” ameongeza Laurent.
Kwa upande wao wakulima wa pamba katika Wilayani Chato wameeleza kufurahishwa na mpango wa ruzuku ya mbolea ulioanzishwa na Serikali, wakisema umeongeza uzalishaji na kuimarisha maisha yao.