WAKULIMA WA PAMBA KISHAPU WAPOKEA MBOLEA ZA KUKUZIA

 Kishapu, Shinyanga,

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bodi ya Pamba na kampuni za mbolea zimewezesha upatikanaji wa mbolea za kukuzia kwa wakulima wa mfano wa Kishapu, mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa uhamasishaji matumizi sahihi ya mbolea kwenye zao la pamba.

Baadhi ya wakulima wawezeshaji wa zao hilo wamepokea mbolea hizo kwa nyakati tofauti na wameeleza kufurahishwa na juhudi za taasisi hizo kuhakikisha mbolea inawafikia kwa wakati. Wametoa shukrani kwa TFRA, Bodi ya Pamba na makampuni ya mbolea kwa ushirikiano wao katika kufanikisha mpango huo.

Joyce George, mkulima wa pamba kutoka Kijiji cha Inolelo, Kata ya Ingofilo, amesema elimu waliyopewa na TFRA kuhusu matumizi sahihi ya mbolea imewasaidia kuona tofauti kubwa katika ukuaji wa zao hilo. Ameeleza kuwa, tofauti na awali walipolima bila mbolea, sasa wana matumaini ya mavuno bora, hali inayowahamasisha kuzingatia kanuni bora za kilimo.

Amesema kuwa matumizi ya mbolea yatawasaidia kupunguza ukubwa wa mashamba na kulima eneo dogo lenye tija kwa kuzingatia kanuni kumi za kilimo bora cha pamba.

Alphonsi Maayunga, mkulima mwezeshaji kutoka Kijiji cha Idushi, amesema kabla ya kutumia mbolea, mavuno yalikuwa hafifu sana, ambapo alikuwa akipata wastani wa kilo 300 kwa ekari moja, kiasi ambacho hakikukidhi mahitaji yake.

Baada ya kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, sasa ana uhakika wa mavuno bora na ameamua kuwaelimisha wakulima wenzake kwa kupanga ratiba ya kuwafundisha mara moja kwa wiki.

Mpango wa uhamasishaji matumizi sahihi ya mbolea kwenye zao la pamba unatarajiwa kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa kilo 300 hadi 900 kwa ekari. Endapo wakulima watazingatia kanuni bora za kilimo, mavuno yanaweza kufikia tani moja na nusu hadi tani mbili na nusu kwa ekari, kulingana na ubora wa ardhi ya shamba husika.

Hatua hii ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji wa pamba nchini na kuinua kipato cha wakulima kupitia matumizi sahihi ya mbolea na mbinu bora za kilimo.



Post a Comment

Previous Post Next Post