UBORESHAJI WA DAFTARI MIKOA YA IRINGA NA MBEYA KUANZA DESEMBA 27 MWAKA HUU

 



Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Desemba 15, 2024 mkoani Mbeya ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao unataraji kuanza Disemba 27 hadi Januari 02,2024. Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila. Na Waandishi wetu Mbeya
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe.Jacobs Mwambegele amesema kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mikoa ya Iringa, Mbeya na Dodoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa umepangwa kuanza tarehe 27 Disemba mwaka huu.

Akifungua Mkutano wa wadau wa uchaguzi katika ukumbi wa Benki Kuu leo jijini Mbeya, ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa uboreshaji wa Daftari katika mikoa hiyo Mhe. Jaji Mwambegele amesema kuwa zoezi hilo litafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 27 Desemba, 2024 na kukamilika tarehe 02 Januari, 2025 na ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

Ameongeza kuwa pindi zoezi la uboreshaji wa Daftari katika mikoa ya Iringa na Mbeya litakapokamilika, Tume itakuwa imekamilisha mzunguko wa nane kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa Daftari.

Aidha, Jaji Mwambegele ameeleza kuwa tangu uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari kufanyika mnamo tarehe 20 Julai, 2024, Tume imekwishakamilisha uboreshaji wa Daftari katika Mikoa 21 nchini.

Mhe. Jaji Mwambegele ameitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida. Mikoa mingine, ni pamoja na Mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba na Kaskazini Pemba iliyopo Zanzibar.

Jaji Mwambegele ameongeza kuwa hivi sasa uboreshaji wa Daftari unafanyika katika mikoa miwili ya Arusha na Kilimanjaro na Tume inatarajia kukamilisha zoezi hilo katika mikoa hiyo mnamo tarehe 17 Desemba, 2024.

Akifungua Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi katika Mkoa wa Iringa, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk amewataka wadau wa uchaguzi kuwahamasisha wananchi wenye sifa za kuandikishwa au wanaotarajia kuhamisha au kuboresha taarifa kwenye maeneo husika watumia fursa hii.

Ameongeza kuwa kufanikiwa kwa uboreshaji wa Daftari, kunategemea sana ushiriki wa wadau wa uchaguzi katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wenye sifa za kuandikishwa au wanaotarajia kuhamisha au kuboresha taarifa zao.

“Hivyo, ni matarajio ya Tume kuwa mtakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili zoezi hili lifanyike kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa,” ameeleza Jaji Mbarouk.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani katika mada yake kwa wadau wa uchaguzi mkoani Mbeya amesema kuwa kwa Mkoa wa Mbeya jumla ya vituo vya kuandikisha wapiga kura 1,577 vitatumika kwenye uboreshaji wa Daftari kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 66 katika vituo 1,511 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.

Mkoani Iringa kuna vituo 1,367 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 140 katika vituo 1,227 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.

Mikutano hiyo ambayo lengo lake ni kupeana taarifa kuhusu hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Tume ili kufanikisha zoezi la uboreshaji wa Daftari imehudhuriwa na Wajumbe wa Tume, Mhe. Asina Omari ambaye alishiriki mkutano huo mkoani Iringa na Mhe. Dkt. Zakia Mohamed Abubakar ambaye alishiriki mkutano wa wadau mkoani Mbeya.







Wadau mbalimbali wa Uchaguzi wakiuliza maswali na kutoa maoni wakati wa kikao hicho.Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Bw. Kailima Ramadhani akitolea majibu hoja mbalimbali za wadau wa uchaguzi.




Wadau wa uchaguzi kutoka Mkoa wa Mbeya wakiwa katika mkutano huo.


Wadau wa uchaguzi kutoka Mkoa wa Mbeya wakiwa katika mkutano huo.



Wadau wa uchaguzi kutoka Mkoa wa Mbeya wakiwa katika mkutano huo.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Dkt. Zakia Mohamed Abubakar akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho.

Post a Comment

Previous Post Next Post