WAONGOZA WATALII WA SAFARI WAPIGWA MSASA JIJINI ARUSHA

 Na. Edmund Salaho/Arusha 

Waongoza watalii wa safari zaidi ya 750 leo tarehe 12, Decemba 2024 wamepigwa msasa katika semina maalum ikiwa na lengo la kujiandaa na msimu mwingine wa Utalii unaoanza Decemba 2024 hadi Februari 2025.

Semina hiyo ya siku mbili inahusisha vyama vya waongoza watalii vya TTGA, NTSGS, TGS, KTGA, IGS, na FGCI imeandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro inafanyika katika ukumbi wa Olasiti jijini, Arusha.

Akifungua semina hiyo ya awamu ya kwanza kwa waongoza watalii hao Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula aliipongeza TANAPA na Ngorongoro kwa kuandaa semina hiyo na kuwaasa waongoza watalii kujivunia kuitangaza Tanzania duniani.

“Tanzania imepata tuzo nyingi duniani ikiwemo tuzo ya Kivutio bora cha Utalii wa Safari duniani ni lazima tujivunie, nisisitize kuendelea kujitolea kuwa bora kwa kuboresha ujuzi wetu, maarifa yetu kuhusu historia ya Taifa letu, Wanyamapori, maeneo ya kihistoria na utamaduni wetu.”

“Utalii unachangia kiasi kikubwa katika uchumi wetu, waongoza watalii ninyi ni mabalozi wa kiuchumi juhudi zenu zinasaidia kuunda ajira, kuimarisha biashara za ndani, na kuinua jamii jivunieni kuwa kiungo muhimu katika mnyororo huu wa maendeleo” 

Aidha, Mabula alisisitiza waongoza watalii kuweka kipaumbele usalama wa wageni,kuboresha huduma na kuweka mazingira mazuri ya ukaribisho katika kila hatua ya safari.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA,  Massana Mwishawa alibainisha kuwa kila mwaka mashirika  ya TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro yamekuwa na utamaduni wa kukutana na wadau wake wa utalii kuweza kutambua na kujadili namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali lakini pia kuendelea kupeana taarifa mbalimbali za maendeleo ya Utalii yanayofanyika katika maeneo yetu ya utalii. 

“Kupitia semina hii waongoza watalii wataendelea  kujenga uelewa wa pamoja juu ya taratibu mbalimbali tulizojiwekea katika hifadhi ili kuwa na utalii endelevu lakini pia kuhakikisha watalii wanaotembelea hifadhi zetu wanapatiwa huduma bora” alisema Kamishna Mwishawa.

Semina hiyo ya siku mbili inahusisha mada mbalimbali kama Huduma Bora kwa wateja, Uzalendo, Ukarimu na Protokali kwa wageni, Changamoto na fursa za Utalii, sambamba na kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali zilizowekwa na Serikali katika maeneo ya utalii.









Post a Comment

Previous Post Next Post