JANA tarehe 1 Desemba 2024, ambapo dunia inaadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani. Kitaifa, maadhimisho haya yamefanyika Mkoani Ruvuma yakiongozwa na mgeni rasmi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Akitoa taarifa yake, Waziri wa Afya nchini, Mheshimiwa Jenista Mhagama, ameeleza juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.
Amesema, Serikali imeendelea kugharamia dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs), hatua inayosaidia wananchi wanaoishi na maambukizi ya virusi hivyo kuendelea na maisha ya kawaida.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, wananchi takriban milioni 1.7 wanaishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini.
Serikali imetumia shilingi bilioni 750 kununua dawa za ARVs, ambapo gharama ya matibabu kwa kila mgonjwa mmoja ni takriban shilingi 400,000 kwa mwaka.
"Maadhimisho haya ni fursa muhimu ya kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI na kupunguza unyanyapaa" amesema Mhe. Jenista
Pamoja na hayo amehimiza jamii kuchukua hatua za kinga na matibabu kwa ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali.
Kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuimarisha mshikamano wa kidunia katika kukomesha maambukizi mapya na kuboresha huduma kwa walioathirika.