Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imejengwa juu ya nguzo tatu kuu, huku akisisitiza kuwa nguzo ya uendelevu wa mazingira ndiyo msingi wa utekelezaji wa nguzo nyingine zote.
Akizungumza Aprili 30, 2026 jijini Dar es Salaam, Kwagilwa alisema nguzo hizo ni uchumi imara, jumuishi na shindani; uwezo wa watu na maendeleo ya jamii; pamoja na uendelevu wa mazingira na ustahimilivu, akibainisha kuwa wataalamu wa mazingira wana jukumu la moja kwa moja kusimamia nguzo hiyo ya tatu.
Alieleza kuwa kufikia mwaka 2050 Tanzania inalenga kuwa na uchumi wa dola trilioni moja pamoja na idadi ya watu kufikia takribani milioni 118, hali itakayoongeza shinikizo kubwa kwa rasilimali za mazingira kama ardhi, maji na misitu.
Kwagilwa alionya kuwa tayari nchi inapoteza takribani hekta laki tatu na sabini za misitu kila mwaka, hivyo akasisitiza umuhimu wa wataalamu wa mazingira kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi hayaathiri uendelevu wa rasilimali hizo.
Alisema ili kufanikisha hilo, tathmini za athari kwa mazingira zinapaswa kufanyika kwa umakini kabla, wakati na baada ya utekelezaji wa miradi, huku akisisitiza kuwa hakuna shughuli inayopaswa kufanyika bila kuzingatia vigezo vya kimazingira.
Aidha, alibainisha kuwa serikali inaendelea kufanya mageuzi makubwa ikiwemo kuandaa marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ili kuimarisha taasisi ya NEMC na kuipa mamlaka kamili zaidi katika kusimamia sekta hiyo.
Alitoa wito kwa wataalamu wa mazingira kupitia TEEA kushiriki kikamilifu katika maboresho ya sheria hiyo ili kuhakikisha inakuwa thabiti na inakidhi mahitaji ya kusimamia uchumi mkubwa unaotarajiwa.
Kuhusu mradi wa makao makuu ya TEEA, Kwagilwa aliutaja kuwa ni wazo sahihi lililokuja kwa wakati muafaka, akisisitiza kuwa wataalamu wa mazingira wanapaswa kuwa na miundombinu inayolingana na uzito wa majukumu yao.
Aliwashauri viongozi wa TEEA kuhakikisha wanalifanyia kazi eneo walilopewa Dodoma kwa haraka ili kuepuka hatari ya kupoteza umiliki, pamoja na kuandaa mpango madhubuti wa utekelezaji wa mradi huo kwa awamu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEEA, Handisi Emmanuel E. Hanai, alisema uzinduzi wa mradi wa TEEA Green Building ni hatua muhimu ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira nchini.
Alisema mradi huo wa makao makuu utakuwa kitovu cha kujengea uwezo wataalamu wa mazingira, hususan vijana, katika masuala ya tathmini za athari za mazingira pamoja na kusaidia kupunguza changamoto ya ajira.
Aidha, Hanai alitoa wito kwa wadau wa mazingira kushiriki kikamilifu katika uchangiaji wa fedha ili kufanikisha mradi huo, akisisitiza kuwa umoja na ushirikiano ni muhimu katika kuijenga sekta hiyo.
Naye Bryan Toshi Bwana, Mwanzilishi na Mfawidhi wa Umoja Conservation Trust (UCT), alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda ili kuimarisha uwezo wa wataalamu wa mazingira barani Afrika.
Bwana alisema Afrika inapoteza fursa nyingi za miradi mikubwa kwa wataalamu wa nje kutokana na kukosa umoja na mikakati madhubuti, akihimiza vyama vya wataalamu kuungana ili kulinda taaluma na kuhakikisha miradi mikubwa inanufaisha wataalamu wa ndani.

