Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linatumia Tamasha la Kimataifa la Maendeleo ya filamu na Sanaa nchini kunadi utalii wa nyika na fukwe kwa washiriki wanaohudhuria tamasha hilo kutembelea Hifadhi za Taifa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
TANAPA iliyojipambanua kwa kauli yake ya *“Ulipo Tupo”* inatumia kusanyiko hilo linalojumuisha watu kutoka mataifa mbalimbali kama fursa muhimu ya kutoa elimu ya uhifadhi, utalii na kunadi fursa za uwekezaji zinazopatikana ndani ya hifadhi hizo.
Wakati wa ufunguzi wa Tamasha hilo la kimataifa Dkt. Gervas Kasiga – Kaimu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania aliitaka TANAPA kuendelea kushirikiana na Baraza la Sanaa na Bodi ya Filamu nchini kwani huendesha matamasha mengi ya kitaifa na kimataifa ambayo ni masoko mazuri ya kutangaza utalii.
“Tunaona wasanii na wanamuziki wengi hutembelea Hifadhi zetu na wengine hufanya “shooting” kuonyesha mandhari nzuri na wanyama wanaopatikana huko. Kitendo hicho huongeza hamasa kwa watalii wengi na wafuasi wa wasanii hao kutembelea maeneo hayo na kuyanadi, tuongeze ushirikiano ili kufikia adhma ya Serikali ya kuongeza idadi ya watalii kupitia sanaa na maonesho”.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Neema Mollel alieleza fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya Hifadhi za Taifa nchini na kuwakaribisha wasanii na watanzania kutoka maeneo mbalimbali nchini kutembelea vivutio hivyo.
“Niwahimize Maprodyuza nguli, wasanii, na watanzania mliopo hapa kuchangamkia fursa kutembelea hifadhi zetu kwani kupitia Kampeni ya *“Shangwe la Sikukuu na TANAPA”* iliyozinduliwa jana Desemba 13, 2024 jijini Arusha, Shirika limekuja na vifurushi vya bei nafuu ambavyo kila mtanzania atamudu kulinga na kipato chake”, aliongeza Kamishna huyo.
Tamasha hilo la Kimataifa la Filamu na Sanaa lililoambatana na maonesho mbalimbali limefunguliwa jana Desemba 13, 2024 katika Viwanja vya Posta Kijitonyama Dar es Salaam.