Wazee ni hazina


 *Siku ya wazee duniani*

Wazee ni hazina

*Na Eben-Ezery Mende*

Oktoba Mosi kila mwaka ni siku ya wazee duniani.

Siku hii hutumika kwa kundi hilo la watu wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea kujadili mambo yanayowahusu na kusherehekea baraka na Neema za kufikia umri huo ambao si binadamu wote wanaobahatika kuufikia.

Mwaka huu kauli mbio inaelekeza namna ambayo inatakiwa kuzingatiwa ili mtu afikiapo uzee aishi kwa furaha.

Kauli hiyo inaeleza, Uzee wa furaha, andaa njia, rekebisha miundombinu kwa starehe uzeeni.

Maisha ya ujana leo ndiyo njia ya kufaidi ama kuteseka ufikiapo uzeeni.

Kazi, mazingira, chakula na mfumo wa maisha ya ujana ndiyo kipimo cha mapumziko mema au mahangaiko mara ufikiapo nyakati za uzee.

Yapo maradhi ya uzee, vyakula vya wazee, mazingira ya kuishi wakati wa uzee na vyote hivyo hutegemea namna ulivyoishi kuanzia utoto, ujana na hatima ya hayo ni uzeeni.

Wakati leo tukiwa tunaiadhimisha siku hii muhimu kwa kundi la wazee tulio kwenye umri wa kuuchungulia uzee tujiulize tuko kwenye njia sahihi ya kuuendea uzee?

Je tukifikia uzee tutamshukuru MUNGU kwa kufikia kundi hilo au titakuwa tunabubujikwa maneno ya laana kwa watoto, ndugu, jamaa, marafiki na majirani kwa kutojiandaa enzi za ujana?

Tukiwa kazini tunatambua kwamba upo wakati uzee utatufika na tutahitaji msaada wa wengine ili kujisaidia ambapo watu hao wanatengenezwa sasa?

Nani ajuae kwamba ataufikia mwisho wa uhai wake (fariki dunia) akiwa kijana au mzee?

Kwa nini usijiandae kuishi maisha ya kutoa maneno ya baraka kila uzungumzapo utakapofikia umri wa uzee?

Wapo wazee ambao watu hutamani kwenda kuwatembelea kwa kuwa wazee hao hutoa maneno ya kuwabariki watu na ili usipitwe na baraka za mwezi au mwaka unawiwa kuwatembelea ili ukachote baraka hizo.

Aidha wapo wazee ambao watu hujiweka mbali nao hawaendi kuwatembelea na kujikuta wakiishi wenyewe kama hawana ndugu, majirani au watu wa ukoo wao kwa kuwa vinywa vyao vimetawaliwa na laana na endapo utawatembelea lazima utaondoka na maneno ya kulaumiwa au kulaaniwa.

Wakati wa kuandaa uzee wako ni sasa. Wakati wa kuandaa wasaidizi watakaokukimbilia utakapozeeka ni sasa.

Ishi kwa tahadhari, upendo, mipango na kuthamini wengine kwa kuwa ulifanyalo leo ni akiba ya kesho.

Kheri kwenu wazee wote MUNGU awajalie maisha marefu tuchote maarifa na baraka kwenu ili tujijenge na kuviandaa vizazi vijavyo vije kuishi kwa usahihi wa utu, ubinadamu na cheko.

Kheri kwako baba yangu, kheri kwako mama yangu. Mwanenu nawapenda nawaombea maisha marefu yasiyo na ndwele yenye tabasamu na furaha tele.

*Dunia bila wazee haijakamilika*

                                       E
                                       B
                                       E
                                 MENDE
                                       E
                                       Z
                                       E
                                       R
                                       Y

Post a Comment

Previous Post Next Post