TRA YAKUSANYA TRILION 7.79 KWA SIKU 90


Kamishna Mkuu TRA Yusuph Mwenda akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba Mosi, 2024 baada ya kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 7.79 ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 105 ya lengo iliyokuwa imejiwekea ya kukusanya Sh. Trilioni 7.42 katika kipindi cha miezi mitatu (julai -Septemba) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.


Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni 7.79 ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 105 ya lengo iliyokuwa imejiwekea ya kukusanya Sh. Trilioni 7.42 katika kipindi cha miezi mitatu (julai -Septemba) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Kamishna Mkuu TRA Yusuph Mwenda amesema ufanisi huo umefanya kuvuka lengo la kila mwezi kwa miezi yote mitatu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba Mosi, 2024 Mwenda amesema katika kipindi cha mwezi Septemba mwaka wa fedha 2024/25, TRAi ilifanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 3.02, sawa na ufanisi wa asilimia 105 ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 2.88.

"Makusanyo haya ni ya kiwango cha juu kabisa cha ukuaji wa asilimia 77.6 kuweza kukusanywa na TRA katika mwezi Septemba, ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2020/21,"amesema Mwenda.

Ameongeza kuwa, ufanisi katika makusanyo yote umechangiwa na maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari nchini kwa kushirikiana na walipakodi, kuwasikiliza na kutatua changamoto zao pamoja na kukua kwa uchumi wa nchi na ongezeko la wawekezaji kutokana na uwepo na usimamizi wa sera nzuri za uwekezaji za serikali ya awamu ya sita.

Aidha amesema sababu nyingine ni kukua kwa ushirikiano na mahusiano kati ya TRA na walipakodi wote nchini kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na ushirikiano mkubwa na mahusiano mazuri wanayoendelea kupokea kutoka kwa viongozi wa vyama vya wafanyabiashara wote nchini.

Amesema, Utendaji kazi mzuri, bidii na kujituma kwa watumishi ikiwemo kuwatembelea walipa katika sehemu zao za biashara siku za mapumziko (Jumamosi na Jumapili) na kutatua changamoto zilizopo kumesaidia katika zoezi hilo kwani ushirikiano huo wa umewezesha zoezi zima la ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Sambamba na hayo, kuendelea kuboresha mahusiano baina ya serikali na wafanyabiashara ikiwemo kutenga siku ya Alhamisi ya kila wiki kuwa ni siku maalum ya Kusikiliza Walipakodi' kupitia ofisi zote za TRA nchini kutaongeza hamasa ya walipa kodi kutimiza wajibu wao kwa hiari.

"Kuongezeka kwa usimamizi wa wafanyakazi kwa kukemea vitendo vya uvunjifu wa maadili ikiwemo kukemea vikali vitendo vya rushwa na kuchukua hatua kwa wanaopatikana na kuthibitika kuhusika katika vitendo hivi, kufuatilia na kuchukua hatua za haraka za kutatua changamoto za walipakodi wanazowasilisha moja kwa moja kwenye ofisi ya Kamishna Mkuu kupitia TRA SIKIKA APP iliyozinduliwa mwezi Agosti 2024," amesema Mwenda

Pia Mwenda amesema kuendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini kwa kuhakikisha marejesho ya madai ya kodi yanafanyika kwa wakati ili kufanikisha fedha hizo kurejeshwa kwenye mzunguko wa shughuli za kiuchumi nchini kumesaidia ongezeko kubwa.

"Kuendelea kutekeleza kwa vitendo maelekezo yaliyotolewa na Serikali ikiwemo la utengenezaji wa mfumo wa kurahisisha ugomboaji wa mizigo inayoingia kwa utaratibu wa ufungishaji wa mizigo (consolidation).Kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini kwa kusimamia kikamilifu bidhaa nane ambazo zimewekewa bei elekezi (vitenge, mashati, nguo zingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti) na ni sababu iliyochangia,"amesema Mwenda.

Amesema jukumu la kufuatilia kwa ukaribu hali ya ufanyaji biashara nchini kwa kusimamia kikamilifu ufanisi wa makusanyo uliofikiwa na TRA kwa miezi ya Julai – Septemba ni kiashiria chanya katika kuhakikisha kuwa lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 la Shilingi Trilioni 30.04 litafikiwa. Katika kufanikisha hilo,Mamlaka ya Mapato Tanzania itaendelea kutekeleza kikamilifu mambo kama vile uzalishaji wa viwandani pamoja na matumizi ya mashine za EFD nchini.

Amesema kuendelea kusimamia utawala wa sheria za kodi kwa haki bila kupendelea wala kumuonea mlipakodi yoyote kumesaidia katika ufanisi huo kwani huweka mazingira ya biashara yaliyo sawa kwa wote.

Alisema jambo jingine ni kuongozeka kwa ufanisi katika usimamizi wa uingizwaji na uondoshwaji wa mizigo katika vituo vyote vya Forodha nchini zikiwemo bandari.

"Katika kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali TRA itaendelea kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi na kusimamia kikamilifu ulipaji wa kodi katika sekta zote.....Pia tutaendelea na zoezi la uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari kwa wananchi na wafanyabiashara ili kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano na walipakodi kupitia utoaji wa huduma bora pamoja na kampeni za elimu kwa mlipakodi.

Pia alisema wataendelea kuimarisha usimamizi wa utoaji wa risiti za kielektroniki za EFD nchini kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji, pamoja na kuwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa utoaji wa risiti za kielektroniki za EFD kwa ajili ya kuleta maendeleo ya nchi.

"Katika hili litafanikiwa endapo tutaendelea na ujenzi na uimarishaji wa mifumo ya kodi za ndani na forodha (IDRAS na TANCIS) inayosomana na mifumo mingine nchini kwa kuendelea kusimamia na kuimarisha misingi ya mfumo mzuri wa kodi, ikiwemo

Haki na Usawa katika utozaji kodi (no favouritism or victimization) ili kuweka mazingira ya biashara yaliyo sawa na kuondoa migogoro.

Pia tutaendelea kushirikiana kikamilifu na timu ilivoteulivwa na Rais ambayo itafanya mapitio ya mfumo wa kodi ili kuleta maboresho makubwa katika mifumo ya kodi nchini,kuimarisha na kusimamia weledi (professionalism) na huduma nzuri kwa

walipakodi (customer service) ikiwemo watumishi wote wa TRA kuvaa vitambulisho wanapotoa huduma.

Mwenda alisema wataendelea kuimarisha vitengo vya Ukaguzi na Uchunguzi wa kodi ili kuzuia ukwepaji kodi za ndani na Forodha, kuondoa upotevu wa mapato ya Serikali ili kuweka mazinigira ya biashara yaliyo sawa kwa wafanyabiashara wote.

Post a Comment

Previous Post Next Post