TFRA yawajengea uwezo vijana wanufaika wa BBT kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo wa thamani wa mbolea

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Mafunzo ya Wizara ya Kilimo kupitia vyuo vya mafunzo vya Wizara ya Kilimo (Ministry of Agriculture Training Institutes - MATIs) imewajengea uwezo Vijana 170 wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow - BBT) katika masuala mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa mbolea. 

Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo tarehe 21 hadi tarehe 22 Septemba, 2024 kwenye kituo cha BBT Chinangali II Jijini Dodoma ambapo vijana hao wamepata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, Sheria ya Mbolea Na. 9 ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2014.

Akifungua mafunzo hayo Dkt. Mashaka Mdangi, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka Wizara ya Kilimo aliyekuwa na majukumu mengine amesema, ni dhahiri kuwa kila mtu anatambua umuhimu wa kilimo katika maisha ya viumbe hai si binadamu tu hata wanyama wa kufungwa kwa sehemu flani wanatengemea malighafi kutoka kwenye kilimo.

Amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kutumia uwezo wao wote kuhakikisha  kilimo kinakua ili kiweze kuchangia katika usalama wa chakula na lishe nchini, kuinua pato la mkulima ili kupunguza umasikini, kuongeza ajira na hatimaye ziada kuuzwa nje ili kuwalisha wengine kibiashara kama dira ya Wizara ya Kilimo inavyofafanua.

“Ili tuweze kukuza kilimo hatuna budi kuhakikisha mimea inapata virutubisho na madini stahiki, vitu hivyo vinapatikana kutoka kwenye mbolea.

"Wataalamu watatoa somo hapa na kila mmoja atamaliza mafunzo akiwa ameiva vizuri” Dkt. Mdangi alisisitiza.

Ameeleza kuwa, fursa iliyotolewa kwa vijana wa BBT na TFRA itakuwa mkombozi kwani mafunzo yanayotolewa yatawasaidia wao pamoja na wakulima wengine watakaosikia shuhuda za kilimo cha kisasa kutoka kwa washiriki wa mafunzo.

“Nimeambiwa kuwa mafunzo haya yanalenga kuwaonesha fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa mbolea ambazo ni pamoja na kufanya biashara ya mbolea na kuwa miongoni mwa wauzaji wa mbolea yaani fertilizer dealers”.  

Dkt. Mdangi ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kuwa makini katika kufuatilia mafunzo na kuwa huru kuuliza maswali ili kujifunza kwa mbinu shirikishi ili kupata uelewa wa eneo lililokuwa halieleweki na kutoka kwenye mafunzo hayo wakiwa wamebobea. 

Amesema, Wizara ya Kilimo inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara ya mbolea ikiwa ni pamoja na uwepo wa takribani ghala 987 zenye uwezo wa kuhifadhi mbolea tani 458,610 nchini.

Mwisho ameiomba TFRA kuona uwezekano wa kufanya mafunzo kama haya kupitia Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vilivyopo nchini na kuendelea kuandaa mafunzo kama hayo kwa vijana wengi wanaojihusisha na kilimo ili kutoa uelewa wa masuala ya mbolea.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa TFRA Kanda ya Kati, Allan Marik amesema, mafunzo yanayotolewa yanajitosheleza katika kumwezesha mshiriki kujihusisha na biashara ya mbolea na kueleza baada ya mafunzo washiriki wote watatunukiwa vyeti vya mafunzo hayo.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye miradi ya kimkakati ili kufikia Agenda 10:30; Kilimo ni Biashara yenye lengo la kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakua kwa asilimia kumi ifikapo mwaka 2030. 

Mada zilizofundishwa kwa siku ya kwanza ni mbolea na visaidizi vya mbolea, Sheria ya Mbolea, kujua virutubisho na makundi ya virutubisho na kazi zake kwenye mmea, kujua makundi ya mbolea zinazopatikana nchini pamoja na kujua aina za mbolea zinazotumika nchini.

Mafunzo hayo yatafungwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent atakayewatunuku vyeti washiriki 170 wa mafunzo hayo.








Post a Comment

Previous Post Next Post