JIJI MBEYA LATAKIWA KUPIMA ARDHI KWA AJILI YA UWEKEZAJI


NA MWANDISHI WETU, MBEYA

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Spika wa Bunge la  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge Duniani, Dkt. Tulia Ackson amesema imefika wakati sasa jiji la Mbeya kuanza kupima ardhi kwa ajili ya uwekezaji badala ya kuendelea kupima viwanja kwa ajili ya makazi lengo likiwa ni kuongeza mapato yatakayotokana na huduma za kijamii.


Mbunge huyo ametoa wito huo leo tarehe 31 Julai, 2024 wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani  kilichofanyika katika Ukumbi wa Mstahiki Meya uliopo kwenye jengo la  Halmashauri ya Jiji la Mbeya chini ya Mstahiki Meya  wa Jiji Mhe. Dor Mohamed Issa.


Dkt. Tulia amesema Jiji la Mbeya linatakiwa kubadilika kwa kuweka maeneo ya uwekezaji ambayo yatawezesha kutoa huduma za kijamii kama vile  mahoteli makubwa, kumbi  kubwa za kisasa za mikutano ambazo zitaongeza  mapato ya Jiji.


Amesema kwa sasa Jiji na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla hauna ukumbi unaoweza kubeba zaidi ya watu 5,000 hivyo kuwa vigumu hata kwa mikutano ya kimataifa kufanyika katika jiji la Mbeya, hivyo ni wakati muafaka kuwekeza katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za ghorofa  kwa ajili ya makazi na biashara.


“Tunashukuru uwanja wa Ndege wa Mbeya umekamilika na ndege za aina yoyote zinaweza kutua , changamoto iliyopo  ni ukosefu wa hoteli kubwa (Five Star Hotels) jambo linalosababisha ndege za kimataifa kutotua uwanja wa Mbeya,” amefafanua Dkt. Tulia. 


Dkt. Tulia amewapongeza Madiwani chini ya uongozi wa Mstahiki Meya pamoja na watendaji wa Halmashauri kutokana na utekelezaji wa majukumu bambalimbali katika kipindi cha mwaka 2023/2024 ambapo wameweza kusimamia vizuri miradi ya maendeleo na usafi wa mazingira na kuliwezesha Jiji kushika nafasi ya pili kwa usafi.


Amesema katika mwaka wa Fedha 2023/2024 suala la elimu lilipewa kipaumbele na kuwezesha ujenzi wa matundu ya vyoo , ujenzi wa madarasa, ukarabati wa majengo ya shule zote za msingi na ununuzi wa madawati mpango ukiwa ni kuziweka  shule zote katika hadhi inayotakiwa na  kuwa mfano wa kuigwa  na Halmashauri nyingine Tanzania.


“Tumejenga matundu 350 ya vyoo mashuleni, kwa mwaka huu wa fedha  matundu 156 ya vyoo yatajengwa na kufanya pungufu ya matundu ya vyoo kuwa 60,” amefafanua Dkt. Tulia.


Aidha Mheshimiwa Dkt. Tulia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.


Mstahiki Meya kwa upande wake amemshukuru Dkt. Tulia kwa jitihada anazofanya kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo jijini Mbeya anafanyika kwani katika mwaka wa fedha 2023/2024  kiasi cha shilingi Bilioni 38.7 zilitolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuhimiza uongozi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa madiwani wanapewa taarifa  pindi fedha za miradi zinapopelekwa katika maeneo yao ili wasimamie kwa ukamilifu.


Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, John Nchimbi amesema kwa mwaka wa Fedha 2024/2025 Halmashauri imetenga kiasi cha Shilingi milioni 871 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo na ukarabati  wa shule zenye changamoto.




Post a Comment

Previous Post Next Post