NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa amemtaka Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dkt. Herbert Makoye kuhakikisha wanaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha Tamasha la Bagamoyo Festival ili liendelee kuwa bora zaidi.
Wito huo ameutoa Oktoba 26, 2024 wakati akifunga Tamasha la 43 la Sanaa na Utamaduni lililofanyika kwa siku nne katika Viwanja wa TaSUBa Bagamoyo mkoani Pwani.
Amesema anataka kuona wasanii mbalimbali wakubwa nchini wakishiriki katika Tamasha lijalo ili liendelee kuwa bora zaidi na kuvutia wageni na wenyeji ambao watakuwa wakishiriki kupata burudani kwenye tamasha.
"Tamasha la 44 la Sanaa na Utamaduni tunataka tuone, wasanii wakubwa wakitumbuiza hapa, katika wale 10 tukipata kuanzia watano itapendeza zaidi". Amesema.
Aidha amesema Serikali inatarajia kuongeza bajeti zaidi kuhakikisha Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), msimu ujao linakuwa bora zaidi.
Amesema kuwa tamasha hilo limekuwa na faida kubwa ikiwemo kutangaza utalii wa Bagamoyo, kutokana na kushirikisha wadau kutoka nchi mbalimbali ambao hupata fursa ya kutembelea vivutio vya Bagamoyo.
“Serikali inatarajia kuongeza bajeti ya hivi sasa katika kuhakikisha tamasha la TaSUBa msimu ujao linakuwa na ubora zaidi. Hata hivyo msimu huu limefanyika kwa ukubwa wake na hii yote ni juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha linakuwa endelevu na lenye ubora ". Amesema Msigwa
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya TaSUBa, Dkt. Herbert Makoye amewashukuru washiriki na wananchi wote waliojitokeza kuhudhuria shughuli hiyo na kuwaahidi kuboresha zaidi katika Tamasha linalofuata la mwakani.
Tamasha hili la Sanaa na Utamaduni, hufanyika kila mwaka katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambapo hukutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Tamasha hili hulenga kukuza vipaji, kuuenzi na kuutunza na kurithisha Utamaduni wetu kwa vizazi vijavyo, kutangaza utalii wa mji wa Bagamoyo, pia kutoa ajira kwa wasanii wa nyanja mbalimbali nchini.