WAZIRI SIMBACHAWENE: HAKUNA KITU KIZURI KAMA MAISHA YA NDOA




Na Mwandishi wetu- Mpwapwa


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene (Mb) amesema maisha ya ndoa ni mazuri huku akimtaka Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mpwapwa
Ndg.Mgutho Thabit Mathew aliyefunga pingu ya maisha na Mke wake Bi. Herieth Kileo kuishi maisha yenye upendo na kujaliana.

Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kama Baba Mzazi wa Ndg. Mghuto kwenye sherehe hiyo iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika Ukumbi wa CCM Wilaya ya Mpwapwa ambapo amewataka wakaishi maisha mema na kuijenga familia yenye heshima.

" Ndoa hii ni ushahidi tosha mbele za watu na mbele za Mwenyezi Mungu, naamini hamtatuangusha na hamfanyi utani tumieni heshima hii ili watu hawa waliokuja hapa wasije kusema walipata hasara na kupoteza muda wao bure" amesisitiza Simbachawene

Amewataka kujiepusha na tabia ya uongo ili waweze kujenga familia yenye ustawi na staha mbele ya jamii na Mwenyezi Mungu.

Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene ametoa wito kwa Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza Mpwapwa katika sekta ya burudani kufuatia uhaba mkubwa wa sehemu hizo hali inayopelekea wakazi wa Mpwapwa kukosa sehemu za kwenda kula maisha.

" Watu wa Mpwapwa wanakosa sehemu ya kwenda kula 'vibe' hivyo uwekezaji wa kipekee unahitajika ili waweze kufurahia maisha " amesisitiza Simbachawene

Ndoa hiyo ya Ndg. Mwenezi Mgutho Thabit Mathew na Ndgu Herieth Kileo ambayo wamefanikiwa kufunga Oktoba 27, 2024 katika Kanisa la Mtakatifu Paulo (St.Paul) wilayani Mpwapwa imehudhuriwa watu wengi akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Dkt.Sophia Kizigo.









Post a Comment

Previous Post Next Post