TAASISI NYINGINE ZIIGE UTENDAJI KAZI WA BRELA: KIGAHE



NA MWANDISHI WETU

NAIBU  Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe ametoa rai kwa taasisi za Serikali kuiga mfano wa utendaji kazi wa Wakala wa Usajili wa Biasahra na Leseni (BRELA) kwa kujipima kupitia maoni ya wadau na si kujifungia na kujitathimini wenyewe maofisini.

Rai hiyo ameitoa leo, Oktoba 25, 204 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa pili wa BRELA na wadau wake wenye lengo la kujadili mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta ya biashara hususan katika eneo la usajili wa leseni za baishara.

“Tangu BRELA walipoandaa Mkutano wa kwanza naamini kuwa kuna maboresho mengi yamefanywa kama Wakala ya Serikali chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zake, nitoe rai kwa taasisi zingine za Serikali ambazo hazina utaratibu huu, kuweza kuiga mfano huu mzuri ili kuweza kujipima kwa kupata maoni na mtazamo kutoka kwa wadau badala ya kujifungia na kujitathmini wenyewe maofisini,”amesema.

Aidha amesema, BRELA haiwezi kufanikiwa kutekeleza majukumu yake ikiwa peke yake, inategema ushirikiano na ukaribu na sekta za umma na binafsi na ndio sababu inafanya mkutano huo kuwa ni muhimu kufanyika ili kufanya tathmini ya wapi taasisi hiyo imetoka, ilipo sasa na wapi inaelekea kwa kukizingatia nafasi yake katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

Ameongeza kuwa ni matarajio yake kuona mkutano huo ambao umeandaliwa na BRELA kwa mara ya pili unakuwa muhimu ili kuifanya taasisi hiyo kuwa taasisi bora na ya mfano katika kutoa huduma bora za sajili na leseni, kutoa elimu kwa jamii ya wafanyabiashara na wawekezaji ili uwekezaji na biashara zinazofanyika ziwe na tija, faida zipatikane kwa wafanyabiashara na Serikali ikusanye kodi kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na uchumi wa nchi uweze kukua na kuimarika.

Pia amesema mkutano huo uwe chachu kwa washiriki na wasambaze elimu kwa wananchi ambao hawajapata fursa ya kuwepo katika mkutano huo kwa maana uelewa wao utapunguza kero mbalimbali na gharama za urasimishaji biashara zitapungua na hatimaye mazingira ya biashara nchini kuwa bora na wezeshi kwani mtu au taasisi yoyote haiwezi kuanzisha biashara bila kuwa imesajiliwa na BRELA au imepata Leseni ya Biashara kwa zile biashara za Kundi “A”.

Ameongeza kuwa anaamini ushiriki wa wadau katika mkutano huo ni ishara kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Dkt Samia Suluhu Hassan za kuweka mazingira bora, wezeshi na shirikishi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini, ukuaji wa biashara na uchumi nchini unaendelea kuimarika na kuweza kufikia malengo ya Serikali katika Mpango wa Maendeleo wa Tanzania wa kufikia uchumi wa kati na endelevu ifikapo mwaka 2025.

Pia amesema nafahamu kuwa tangu mwaka 2018 BRELA imekuwa ikitoa huduma zake za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kupitia mifumo ya Usajili kwa njia ya Mtandao (Online Registration System) na Dirisha la Taifa la Biashara (Tanzania National Business Portal).

Hivyo kupitia mifumo hiyo imefanikiwa kupunguza muda, gharama na bughudha kwa wawekezaji na wafanyabiashara ambao walikuwa wanasafiri umbali mrefu kufika katika Ofisi za BRELA Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma hizo. 

 

“Utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao umerahisisha mambo ambapo wafanyabiashara wanaweza kuomba kusajili au kupata Leseni za Biashara zao wakiwa maofisini kwao na wakapata cheti cha Usajili au Leseni pale pale alipo bila kuhitaji kufika katika ofisi za BRELA.

Pia amesema Serikali imefarijika na taarifa ya maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji iliyotolewa na Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji katika mkutano wa uzinduzi wa taarifa hiyo Septemba 11, 2024 jijini Dar es Salaam na zaidi ilipoelezwa kwamba moja ya mafanikio ya maboresho hayo ni pamoja na BRELA kuweza kusajili kampuni na majina ya Biashara pamoja na kutoa Leseni za Biashara ndani ya siku moja.

“Hii ni hatua kubwa katika uboreshaji wa mazingira ya biashara na imetokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara na taasisi zake katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

 

Pamoja na mambo mengine Kigahe alitoa rai kwa kuwa taka Brela wasibweteke na maboresho hayo ya kimfumo kwani Teknolojia inabadilika kila siku, hivyo muweke mkakati wa kuhakikisha mnakwenda sambamba na maboresho ya kiteknolojia ili huduma zao zizidi kuwa bora na wezeshi.

 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela ,Godfrey Nyaisa kwa upande wake ameishukuru Wizara ya Viwanda na Biashara hasa watumishi, wakiongozwa na Katibu Mkuu Dk.Hashil Abadallah kwa ushirikiano na miongozo ambayo wamekuwa wakiwapa, ushirikiano huo umewezesha kutimiza majukumu yeo kwa ufanisi na kwa weledi, lengo likiwa ni kuhakikisha BRELA inatoa huduma bora na kwa wakati. 

 

Nyaisa amesema,Wizara hiyo imekuwa kiungo muhimu kwao kwa kusaidia na kuhakikisha BRELA inakuwa na mifumo na nyaraka mbalimbali za kiutendaji kazi.

 

 

Amesema kwenye mkutano wa mwaka jana, Wizara ilitoa maelekezo mahususi kwa BRELA, kuwa mkutano huo uwe unafanyika kila mwaka na BRELA iandae majibu na mpango wa utekelezaji wa maoni, ushauri na mapendekezo ya wadau.

 Ameongeza kuwa maelekezo hayo yalipokelewa na kufanyiwa kazi, ndiyo maana wameandaa mkutano huu wa pili na wadau wake ambao utatoa majawabu ya utekelezaji wa maoni, ushauri na mapendekezo ya wadau ya mwaka jana.

Amesisitiza kuwa jambo hilo ni moja ya kigezo kinachotoa taswira ya BRELA kuchukulia maoni ya wadau kwa uzito mkubwa, na pia hii ni sehemu ya uwajibikaji wa moja kwa moja kwa wadau wao.

” Kauli Mbiu ya Mkutano wa Mwaka huu ni “Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation). Wote ni mashaidi kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mama yetu Mpendwa Samia Suluhu Hassan, amekuwa akitoa maelekezo na miongozo ya Mifumo ya Taasisi za Serikali kusomana. Lengo ni kurahisisha utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara kwa ujumla.

 

“Washiriki wengi wanaijua historia ndefu ya BRELA toka ikiwa Idara ndani ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ikijulikana kama “Ofisi ya Msajili wa Makampuni” mbali na kuwa ilikuwa ikitoa huduma za sajili zikiwa ni pamoja na Majina ya Biashara “Business Names”, Alama za Biashara na Huduma “Trade and Service Marks, Hataza “Patents” na utoaji wa Leseni za Viwanda “Industrial Licenses”.

 

“Mageuzi makubwa yalianza kufanyika Desemba 3, 1999, baada ya BRELA kuwa Wakala wa Serikali chini ya Sheria ya Wakala za Serikali “Executive Agency Act No. 30 of 1997”. Mabadiliko haya yalilenga kuharakisha utoaji huduma na kuboresha mazingira ya utendaji kazi. Wengi wenu ni mashahidi kuwa bado mabadiliko hayo hayakukidhi kiu zenu. Mifano midogo tu, usajili wa kampuni ulitoka miezi mitatu au wiki mbili, upatikanaji wa majalada bado ulikuwa changamoto kubwa, mazingira ya ofisi yalikuwa na mchanganyiko na ofisi nyingine binafsi, lakini pia vishoka walitumia fursa hii kufanya ulaghai na wengine kujifanya kuwa ni watumishi wa BRELA.”, amesema. 



Post a Comment

Previous Post Next Post