TANZANIA YANG’ARA KIMATAIFA PROGRAMU YA KIZAZI CHENYE USAWA

 Na Mwandishi Wetu,

Tanzania imekuwa kinara katika programu ya kizazi chenye usawa ambapo imechaguliwa kuingia katika bodi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusu wanawake (UN WOMEN) kati ya nchi saba (7) duniani zilizochaguliwa kuingia, huku Tanzania na Afrika Kusini ndo nchi pekee katika Bodi hiyo kutoka Bara la Afrika.

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 2, 2024 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Ushauri wa Utekelezaji wa Ahadi za nchi katika Jukwaa la kizazi cha usawa akiwa kwenye  mkutano wa Afrika wa Jukwaa la Wanawake viongozi (African Women Leaders Network-AWLN) ambapo huungana kujadili masuala mbalimbali ili kuendeleza malengo ya Jukwaa hilo Tanzania na Afrika.

“Ni fursa nzuri kwetu kuendelea kufanya tathmini ambapo tumebakiza miaka miwili kukamilisha mpango huu naomba  nitoe habari njema kwa Watanzania kwamba kupitia kinara wetu Mkuu Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miaka hiyo mitatu tangu tumeanza kupeleka ripoti Umoja wa Mataifa ni asilimia 31 tu ya ripoti zilizokuwa zinapelekwa na Tanzania pia ni mojawapo  ya nchi ambayo tulipigiwa mfano  na tumeweza kuingia katika bodi ya Shirika la umoja wa Mataifa” amesisitiza Waziri Kairuki.

Amefafanua kuwa ushindi huo unatokana na kazi nzuri ya Mhe. Rais na pia kazi za Tanzania kuonekana Kimataifa  ambapo ina afua mbalimbali zinazotekeleza programu ya kizazi chenye usawa wa kijinsia akitolea mfano wa afua za afya, elimu bure, nishati safi ya kupikia, maji, na kadhalika.

“Mmeona la nishati safi ya kupikia lakini afua za afya, elimu bure na mambo mengine lakini bila kumsahau Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye pia tulipompelekea programu hii ya jukwaa la kizazi chenye usawa alilipokea vizuri lilienda mpaka kwenye Baraza la Mawaziri likapitishwa kama ambavyo lilipitishwa huku Bara ambayo sasa ni program  ya kitaifa” Mhe. Kairuki amesema.

Amesema kupitia jukwaa hilo Wizara zote zinazotakiwa kutekeleza afua husika zinafuatiliwa  akitolea mfano Wizara ya Nishati ambayo inatakiwa kutekeleza upatikanaji wa umeme vijijini, Wizara ya Mawasiliano kuhakikisha kila Mtanzania anaweza kupata mawasiliano, Wizara ya Maji, Wizara ya Fedha kuhakikisha mitaji inapatikana kwa unafuu na Wizara ya Kilimo kuhakikisha  upatikanaji wa mbegu, pembejeo, viuatilifu kwa wanawake vijana na makundi mengine na masoko kupitia teknolojia.

Ameweka bayana kuwa kati ya maeneo sita, Rais Samia aliona ni vyema akachagua eneo la haki za usawa wa kiuchumi kwa wanawake kwa sababu kupitia eneo hilo, Watanzania wamejikomboa kiuchumi, kielimu, afya, masuala ya kijamii, utunzaji wa mazingira ,teknolojia na mambo kadhalika.

Amesema Tanzania imeshiriki katika kutoa taarifa mbalimbali kwa miaka mitatu ya programu hii ya jukwaa la kizazi  chenye usawa ambayo itakamilika Julai 2026.

Mtandao wa Jukwaa la Viongozi Wanawake wa Kiafrika (African Women Leaders Network-AWLN) uzinduliwa mwezi Juni mwaka 2017 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Jukwaa la Kizazi cha Usawa  ni programu inayoongoza duniani kuharakisha uwekezaji na utekelezaji wa usawa wa kijinsia.



Post a Comment

Previous Post Next Post