KUELEKEA MIAKA 60 YA HIFADHI YA TAIFA MIKUMI ROYAL TOUR YATAJWA KUKUZA UTALII

 *Mafuru aeleza mikakati ya TTB katika kukuza sekta ya Utalii


LICHA Ya kuwa mbuga kinara inayotembelewa zaidi na watalii kutoka ndani ya Nchi, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi Agosti itatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake huku juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour zikielezwa kukuza zaidi Utalii katika hifadhi hiyo yenye miundombinu rafiki inayowawezesha watalii kutumia magari binafsi kufanya Utalii, malazi ya kutosha pamoja na vivutio vya kutosha.

Akizungumza katika kikao kazi kilichoikutanisha Bodi ya Utalii Tanzania (TTB,) pamoja na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika Hifadhi ya Mikumi mkoani Morogoro Kamishina wa Uhifadhi Mikumi Agustino Masesa alieleza kuwa; Miundombinu ya hifadhi hiyo imekuwa ikivutia watalii kutoka mikoa mbalimbali nchini pamoja na visiwani Zanzibar ambao hutembelea hifadhi hiyo kupitia uwanja wa ndege uliopo katika hifadhi hiyo.

"Kupitia Royal Tour iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan watalii wengi wamekuwa wakitembelea hifadhi hii kutokea Zanzibar kupitia uwanja wa ndege, Tunapokea watalii zaidi ya 150 kwa siku kupitia uwanja wa ndege haya ni mafanikio makubwa katika sekta ya Utalii." Alieleza.

Aidha Masema alifafanua kuwa, kuanza kwa usafiri wa reli ya kisasa (SGR,) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro umeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya Utalii ambapo watalii wengi wamekuwa wakitembelea hifadhi hiyo kwa kutumia usafiri wa treni ya mwendokasi hasa mwisho mwa wiki.

"Miundombinu inavutia soko la utalii, wageni kutoka Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mbeya na Tunduma; Tunapokea wageni takribani 300 kwa siku, watalii wakitoka kubarizi katika fukwe Zanzibar wanakuja Mikumi kwa ajili ya game drive.....Tupo tayari kuwapokea wageni wengi zaidi na kutoa huduma bora kwa ustawi wa Taifa."

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB,) Ephraim Balozi Mafuru alieleza mikakati ya Bodi kwa kushiriki na Wizara ya Maliasili na Utalii ni pamoja na Bodi hiyo kujitegemea kwa kutengeneza vyanzo vya fedha.

"Kupitia mazao mbalimbali ya utalii ikiwemo utalii wa mikutano ujenzi wa kituo cha Mount Kilimanjaro International Convention Center (MKICC,) chenye ukubwa wa kubeba washiriki takribani 3000, eneo la maonesho lenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 10,000 pamoja na eneo la hoteli za kitalii hivi vitasaidia kuinua na kuingiza kipato.

Pia ameeleza mikakati mingine ni pamoja na kushirikiana na wadau wa Utalii zikiwemo Wizara, vyombo vya habari, Balozi, mashirika ya ndege na taasisi za utalii katika kutangaza vivutio, kubidhaisha vivutio katika masoko ya kitaifa na kimataifa na kuwekeza katika sekta hiyo katika usafiri, malazi, shughuli za kitalii pamoja na vivutio.

Aidha alieleza kuwa Bodi hiyo itatumia viwanja inavyomiliki katika jiji la Dar es Salaam kujenga vitega uchumi mbalimbali ili TTB iweze kujitegemea kifedha pamoja na kuhakikisha kuwa fursa zote za utalii nchini kuanzia ngazi ya Halmashauri zinatambulika na kufanyiwa kazi ili ziweze kuliingizia Taifa kipato.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo Cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii John Mapepele alieleza sekta ya Utalii imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa na katika kuiendeleza zaidi wataendelea kukutana na wadau mbalimbali ili kuendelea kukuza sekta hiyo muhimu yenye vivutio vingi na vipekee ulimwenguni ikiwemo
hifadhi za nyuki ambapo 2027 Tanzania itaandaa jukwaa la utalii wa nyuki itakayokutanisha washiriki wapatao elfu saba na kunufaika na Teknolojia kutoka mataifa mbalimbali, malikale, makumbushao ya Taifa na utalii wa maji.

"Wahariri ni kundi muhimu sana na tumekutana hapa ili kuwapa uelewa zaidi wa mazao mapya na mengi ya Utalii ili waweze kuyatangaza kupitia vyombo vyao vya habari." Amesema.

Juni 3, mwaka huu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha bajeti ya jumla ya shilingi Bilioni mia tatu arobaini na nane milioni mia moja ishirini na tano na laki nne na kumi na tisa elfu (348,125,419,000,)ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
 

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB,) Ephraim Balozi Mafuru akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza mikakati ya Bodi  kwa kushiriki na Wizara ya Maliasili na Utalii ni pamoja na  Bodi hiyo kujitegemea kwa kutengeneza vyanzo vya fedha.
 

Mkuu wa kitengo Cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii John Mapepele akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa sekta ya Utalii imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa na katika kuiendeleza zaidi wataendelea kukutana na wadau mbalimbali ili kuendelea kukuza sekta hiyo muhimu.
 Kamishina wa Uhifadhi Mikumi Agustino Masesa akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa Miundombinu ya hifadhi hiyo imekuwa ikivutia watalii kutoka mikoa mbalimbali nchini pamoja na visiwani Zanzibar ambao hutembelea hifadhi hiyo kupitia uwanja wa ndege uliopo katika hifadhi hiyo.

 

Matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo.

Post a Comment

Previous Post Next Post