WAZIRI SIMBACHAWENE: DIWANI MHE. MARIA KIGOSI HAKUPEWA SUMU,KIFO CHAKE NI CHA KAWAIDA

 Mwandishi Wetu,

Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe.George Simbachawene amesema aliyekuwa Diwani wa Viti Maalum wa Jimbo la Kibakwe, Mhe.Maria Kigosi amekufa kifo cha kawaida na hakuna mtu yeyote aliyempa sumu.

Pia, amesema Marehemu hajafa kifo cha ghafla kama inavyodaiwa bali alikuwa anaumwa na amefia hospitali ya Tumaini Wilayani Mpwapwa.

Ametoa kauli hiyo leo  wakati akishiriki Ibada ya mazishi iliyofanyika katika  Kanisa Katoliki Parokia ya Kibakwe, Tarafa ya Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya  Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Amefafanua kuwa Marehemu alikuwa anaumwa kwa muda mrefu ambapo watu wa karibu akiwemo Mume wa Marehemu anatambua kuwa Mke wake alikuwa akiumwa kwa muda mrefu na amekiri kuwa  alikuwa mbioni kumpeleka Mke wake katika hospitali kubwa.

‘‘ Lakini huku mtaani  kumekuwa na   maneno mengi kuwa Marehemu alipewa sumu na wameenda mbali zaidi kwa kuwataja  wahusika waliompa sumu na  sumu hiyo ilitoka kwa nani,  nataka niwahakikishie sio kweli ni huo uongo mtupu " ameng’aka Mhe. Simbachawene

Amesema kuna wengine wameanza kuthubutu hata kuwataja wahusika waliompa sumu hiyo huku akisisitiza wenye tabia hiyo waache mara moja kwani huo na hautawasaidia chochote

Aidha, ameweka bayana kuwa Serikali imefanya utafiti wake kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na familia yake hususani mume wake na  kujiridhisha kuwa Marehemu Maria hakulishwa sumu.

Hata hivyo Mhe.Simbachawene amesema madaktari wameweza kujua alichokuwa akiumwa ndani ya muda mfupi aliokimbizwa hospitalini.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Simbachawene amewataka Madiwani,  Wananchi wa Kibakwe pamoja na familia yake kwa ujumla  kupuuza uvumi huo la sivyo wataanza kugombana pamoja na kudhalilishana kwenye jambo lisilo na chembe chembe yoyote ya ukweli.

" Tutagawanyika, tutavunja umoja wetu tulioujenga kwa muda mrefu na tutaruhusu maadui kuingia bila sababu nataka niwahakikishie Maria ameondoka kwa kifo cha kawaida.

 Mhe. Simbachawene amemuelezea Diwani Maria kama Kiongozi aliyependa kuunganisha watu na kuwaasa viongozi wengine kuna kitu cha kujifunza kutoka kwake.

Pia ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa familia, Uongozi wa Chama  cha Mapinduzi wilaya ya Mpwapwa, pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kwa kuondokewa na Kiongozi mahiri.

 Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mhe, Maria Kigosi alifikwa na umauti siku ya jumatano saa kumi usiku mara baada ya kuanza kujisikia vibaya na kukimbizwa hospitalini ya Tumaini Wilayani Mpwapwa alikoenda kwa ajili ya kushiriki vikao vya Madiwani.






Post a Comment

Previous Post Next Post