TBS YASISITIZA WAFANYABIASHARA KUZINGATIA VIWANGO

 Raisa Said, Tanga


Shirika la Viwango Tanzania (TBS ) limesisitiza wafanyabiashara kuzingatia bidhaa zao zimekidhi matakwa ya viwango kwani kwa wale wasiofuata taratibu hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kupigwa faini kuanzia million 10 hadi million 100.

Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano na Masoko TBS Gladness Kaseka wakati akizungumza na waandishi wa habari na Wadau waliofika katika banda lao lililopo kwenye maonyesho ya 11 ya biashara na utalii yanayofanyika viwanja vya Usagara Jijini Tanga.

Kaseka ameeleza kuwa taarifa zilizopo kwenye vifungashio za bidhaa zinaumuhimu haswa katika bidhaa za chakula kwa kuwa zinampa taarifa ya usalama mtumiaji wa mwisho ambazo zitamfanya kuwa na uhakika wa kitu anachotumia.

Pia alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuhakikisha wanasoma taarifa zilizopo kwenye bidhaa wanazo nunua kujua viambata vilivyopo na kama zimethibitishwa au la ili kuepuka hasara yoyote wanayoweza kuipata kwa kutumia bidhaa zilizo chini ya kiwango

"Ukikutwa unauza bidhaa hafifu unaweza kupigwa faini si chini ya sh.10 million lakini isiyozidi million 100 inategemea na kosa lako utakalokutwa nalo kwa wakati huo kwasababu Kuna mwingine unakuta bidhaa ilikuwa ni bora lakini imekosa Ubora kwa kuisha muda wake" Alieleza Meneja huyo Wa Uhusiano na Masoko kutoka TBS .

" Bidhaa zote za ziwe zinazalishwa ndani au zinatoka nje ya nchi zinatakiwa ziwe na Ubora kwani TBS tunazikagua zote zinazoingia katika mipaka na zinazozalishwa ndani ya nchi ( viwandani) hivyo epukeni kutumia bidhaa ambazo hazijathibitishwa ubora wake na TBS" Amesisitiza Kaseka

Hata hivyo Ofisa Udhibiti Ubora kutoka TBS Kanda ya Kaskazini, Beatus Mfyomi alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wafike kwenye Banda lao ili waweze kupatiwa elimu kuhusu masuala ya ubora na usalama wa bidhaa.

Maonesho ya biashara na utalii hufanyika kila Mwaka Jijini Tanga na hushirikisha taasisi na mashirika mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post